Trending News

CCM Adverts and Promo

Tuesday, January 17, 2017

Mwenyekiti wa Tume Mhe. Jaji (R) Semistocles Kaijage atembelea kata ya Ngh'ambi kukagua mwenendo wa Uchaguzi Mdogo

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mpwapwa Bw. Mohamed Maje (kulia) akimueleza jambo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (katikati) na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume Bw. Emmanuel Kawishe baada ya kikao cha kupokea taarifa ya mwenendo wa Uchaguzi Mdogo wa Kata ya Ngh’ambi.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (aliyevaa kofia nyeusi)  akipokea maelezo kuhusu mabango ya Uchaguzi kutoka kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Ngh’ambi James Mkinga (wa tatu kushoto) wakati alipokuwa akikagua mabango hayo nje ya kituo cha kupigia kura cha Kata ya Ngh’ambi kilichopo kwenye Zahanati ya Ngh’ambi.

Na. Hussein Makame -Mpwapwa, DODOMA.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji (R) Semistocles Kaijage amesema kila kitu kiko sawa tayari kwa uchaguzi mdogo wa kumpata diwani wa kata ya Ngh’ambi iliyoko katika halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Mhe. Jaji (R) Kaijage ameyasema hayo kutokana na kuridhishwa na maandalizi ya uchaguzi mdogo wa kata ya Ngah’ambi baada ya kutembelea na kufuatilia mwenendo wa uchaguzi wa kata hiyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 22 Januari mwaka huu.

Akitoa taarifa fupi ya mwenendo wa uchaguzi mdogo wa kata hiyo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mpwapwa Bw. Mohamed Maje alisema karibu vifaa vyote kwa ajili ya uchaguzi huo vimepokelewa na kampeni za uchaguzi huo zinaendelea kwa amani na utulivu.

Alisema baada ya uteuzi wa wagombea kufanyika Desemba 22 mwaka 2016 wagombea wanne kutoka vyama vya ADC, CCM, CHADEMA na CUF waliteuliwa ambao ni David Mazengo, Richard Kaleme, Leornard Majenda na Hassan Kiuka, mtawalia.

Kwa upande wa pingamizi kwa wagombea, Bw. Maje alisema walipokea pingamizi kutoka vyama vya CHADEMA na CCM ambapo mgombea wa CHADEMA alipinga uteuzi wa mgombea wa CCM kwa madai kuwa si mkazi wa halmashauri husika.

“Pingamizi hili lilitolewa uamuzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata kwa kutupilia mbali madai hayo baada ya uthibitisho kuwa mgombea wa CCM ni mkazi halali wa halmashauri husika.Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo pia alikubaliana na uamuzi wa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata.” alisema Bw. Maje na kuongeza kuwa:

“Mgombea wa chama cha CCM alipinga uteuzi wa mgombea wa chama cha CHADEMA kuwa fomu ya uteuzi namba 8 C sehemu C na D imesainiwa na mtu ambaye si Katibu wa chama husika wa mkoa au Wilaya”

“Pingamizi hili pia lilitolewa uamuzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata kwa kutupilia mbali madai hayo baada ya uthibitisho wa maandishi kuwa aliyesaini ndiye Katibu wa chama husika wilaya ya Mpwapwa.Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo alikubaliana na uamuzi huo”

Aliongeza kuwa kamati za maadili kwa ngazi ya jimbo na kata zinafanya kazi na kwamba hadi kufukia Januria 13 kamati hazikupokea malalamiko yoyote kutoka kwenye vyama vinavyoshiriki uchaguzi mdogo kata hiyo.

Alisema wanatarajia kutoa mafunzo kwa makarani waongozaji na wasimamizi wa vituo vya kupigia kura tarehe 18 na 19 Januari na wameshaandaa vituo 12 vya kupigia kura vyenye wapiga kura 4123.

Kwa upande wa Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Mpwapwa OCD Hussein Mdoe alisema hadi sasa kampeni zinafanyika kwa kuzingatia taratibu za nchi na taratibu za uchaguzi na hakuna vurugu zozote zilizojitokeza.

Hata hivyo aliwakumbusha wananchi kuwa jukumu la ulinzi na usalama ni la kila mwananchi na anaamini wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa kata na kamati za maadili zitawakumbusha wananchi jukumu hilo.

Kwa upande wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Ngh’ambi Bw. James Mkinga alisema maandalizi yote ya uchaguzi yamekamilika na wameshabandika daftari la kudumu la wapiga kura kwenye vituo vya kupigia kura.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe aliwakumbusha wasimamizi wasaidizi kuhakikisha Sheria, kanuni na taratibu zote za Uchaguzi zinazingatiwa.
Aliwataka wawakumbushe wananchi kufika kwenye vituo vya kupigia kura kwa wakati ili kuepuka kukosa haki ya kupiga kura kwa sababu ya kuchelewa kufika kituoni.
“Hakikisha mnavikumbusha vyama vyote kuondoa mabango ya kampeni yaliyopo kituoni siku ya kupiga kura na kama hawawezi kuyaondoa uwafahamishe kwamba utayaondoa kwa sababu sheria inakataza” alisema Bw. Kawishe na kuongeza kuwa:
“Wakumbusheni wasimamizi wa vituo kufuata Sheria, kanuni na taratibu na yeyote atakayekiuka Sheria Tume ya Taifa ya Uchaguzi haitasita kumchukulia hatua za Kisheria” 
Aliwakumbusha kuhakikisha kuwa mawakala wa vyama wanafuata taratibu zote inapotokea chama kinataka kumbadilisha wakala kwenye kituo cha kupigia kura.
Naye Mkuu wa Kanda ya Kati ya Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bi. Saada Kangeta aliwakumbusha wasimamizi wasaidizi kuwa iwapo litajitokeza jambo linaloweza kuchelewesha matokeo kama kufanya uamuzi ya kura za mgogoro wawafahamishe wananchi ili kuepuka vurugu.

HAKUNA BAA LA NJAA NCHINI - WZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema nchi haijakumbwa na baa la njaa na amewataka Watanzania utosikiliza kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiasha kuhusu hali ya chakula kwani si za kweli bali ni za uzushi zenye lengo la kupandisha bei za vyakula.


Amesema Serikali ndio yenye jukumu la kutoa taarifa za kuwepo kwa njaa ama kutokuwepo na kwamba taarifa zinazosambazwa za kuwepo kwa baa la njaa nchini hazina ukweli wowote na Serikali inawahakikishia wananchi kuwepo kwa usalama wa chakula.



Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo(Jumatatu, Januari 16, 2017) wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa mara baada ya kuzindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, ambapo amesisitiza kwamba hali ya upatikanaji chakula nchini ni tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari.



Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya kutolewa kwa taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu kuwepo kwa baa la njaa nchini jambo ambalo si la kweli. Amewataka wananchi kuwa watulivu na jambo hilo likitokea Serikali itatoa taarifa.



“Mwaka jana nchi ilikuwa na akiba ya chakula cha zaidi ya tani milioni tatuhali iliyopelekea baadhi ya Wabunge na wafanyabiashara kuomba kibali cha kuuza nafaka nje ya nchi, ambapo Serikali ilitoa kibali hicho baada ya kujiridhisha kuwepo kwa akiba ya kutosha ya chakula,” amesema.



Amesema baada ya kutolewa kwa kibali hicho tani milioni 1.5 ziliuzwa nje ya nchi na



Kiasi cha tani milioni 1.5 zilizobaki zilihifadhiwa kama akiba ambapo tayari wameruhusu ziuzwe hapa nchini ili kupunguza kupanda kwa bei za vyakula nchini.



“Naomba wananchi msiwe na wasiwasi juu ya hali ya chakula nchini. Msisikilize kelele zinazopigwa na watu mbalimbali pamoja kwenye baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo magazeti kwani taarifa hizo si za kweli. Chakula kipo cha kutosha licha ya mvua kusuasua katika baadhi ya maeneo nchini,” amesema.



Hata hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa kwa sasa mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo amewaomba wananchi kuzitumia kwa kulima mazao ya muda mfupi yanayostahimili ukame.



Waziri Mkuu amesema kwamba endapo kutatokea uhaba wa chakula nchini, Serikali itatoa utaratibu wa namna ya upatikanaji wa chakula kwa wananchi wake. Kuhusu kupanda wa bei ya vyakula katika baadhi ya masoko amesema inatokana na kuwepo kwa uhaba wa chakula katika nchi jirani.



Aidha, Waziri Mkuu amesema kwamba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, itatoa taarifa kuhusiana na hali halisi ya chakula nchini kwa sasa na pia itatoa taarifa kuhusu hali ya mvua ili Watanzania waweze kupata ukweli wa hali ilivyo.




IMETOLEWA NA:



OFISI YA WAZIRI MKUU,



S. L. P. 980,



DODOMA.  




Friday, January 13, 2017

RAIS DKT. MAGUFULI AFUNGUA VIWANDA VIWILI MKOANI SHINYANGA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe magufuli akikata utepe kuashiria kufungua rasmi Kiwanda cha kutengeneza mifuko ya Sandarusi cha Fresho Investment Compaany limited cha Mkoani Shinyanga. Wengine katika picha ni mkuu wa mkoa wa Shinyanga  Zainabu Taleck wakwanza kulia mwenye kilemba , mbunge wa Shinyanga mjini Stephen Masele wakwanza kushoto, pamoja na mmiliki wa kiwanda hicho Fred Shoo watano kutoka kulia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe magufuli akivuta utepe kwenye jiwe la ufunguzi wa kiwanda hicho cha kutengeneza mifuko ya Sandarusi cha Fresho Investment Compaany limited cha Mkoani Shinyanga. Kulia ni mmiliki wa Kiwanda hicho Fred Shoo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe magufuli akiangalia moja ya hatua za mwisho katika utengenezaaji wa mifuko ya Sandarusi katika kiwanda hicho cha Fresho mkoani Shinyanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe magufuli akiwa amechuchumaa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali pamoja na wafanyakazi wa Kiwanda hicho cha Kutengeneza mifuko ya Sandarusi mkoani Shinyanga.PICHA/IKULU.

NEC YATOA UFAFANUZI WA MALALAMIKO YA UKIUKWAJI WA MAADILI YA UCHAGUZI YALIYOTOLEWA NA ACT-WAZALENDO.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima akitoa Ufafanuzi kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi yaliyotolewa na Chama cha ACT WAZALENDO

13/1/2017. Dar es Salaam.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekishauri Chama cha ACT – Wazalendo na Vyama vingine vyenye wagombea wa Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Dimani na Udiwani katika Kata Ishirini (20) za Tanzania Bara ,kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi kwenye Kamati za Maadili zilizo katika maeneo yao.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Kailima Ramadhan amesema NEC imepata taarifa kupitia Vyombo mbalimbali juu ya malalamiko ya Chama Cha ACT-Wazalendo kuvilalamikia Vyombo vya Dola pamoja na Watendaji wa Umma kufanya vitendo vyenye muelekeo wa kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Bw. Kailima amesema taarifa ya Chama hicho iliyotolewa kwenye Vyombo vya Habari Januari, 12 2017, imeeleza kuwa Watendaji wa Halmashauri ya Geita waliwakusanya Wazee katika Kata ya Nkoma waje na Vitambulisho vyao vya kupigia Kura kwa lengo la kuwapatia huduma ya afya bure jambo linalolalamikiwa na ACT- Wazalendo kwa madai kwamba Watendaji hao wana lengo la kuwahadaa Wazee hao ili wakipigie Kura Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, amesema katika malalamiko yake Chama cha ACT Wazalendo kimeibua tuhuma za wananchi kupokwa kadi za kupigia Kura ili wasiweze kushiriki katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 22, 2017.
Mkurugenzi Kailima amesisitiza kuwa ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 mtu kumiliki kadi ya kupigia kura isiyokuwa yake.
“Natoa wito kwa wananchi wote kwamba, ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 mtu yeyote kumiliki kadi ya kupigia kura isiyokuwa yake”  Amesema.
Amefafanua kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa  kuzingatia sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi inavikumbusha Vyama vya Siasa kuwa iwapo vitakuwa na malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani viwasilishe malalamiko hayo kwenye Kamati ya Maadili ngazi ya Kata ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio linalolalamikiwa.
“ Sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi yayosainiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Serikali na Vyama Vya Siasa inaeleza wazi muda wa kuwasilisha malalamiko kwa kuvitaka vyama au wahusika wenye malalamiko yoyote  kuyawasilisha kwa maandishi kwenye Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya ngazi husika ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio” Amesisitiza Kailima.
Amesisitiza kuwa iwapo Chama cha Siasa au Mgombea hataridhika na maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Kata, kwa kuzingatia sehemu ya 5.7 (a) ya Maadili ya Uchaguzi anatakiwa awasilishe rufaa yake kwa Msimamzi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo ndani ya saa 24 tangu maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya kata kutolewa.
Aidha, Bw. Kailima amebainisha kuwa kama Chama cha Siasa hakikuridhika na maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo, bado kwa kuzingatia sehemu ya 5.7 (b) na (c) kinayo fursa ya kuwasilisha Rufaa yake katika Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa au ngazi ya Rufaa ambayo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“ Tunavishauri Vyama vya Siasa na Wagombea kuzingatia matakwa ya Maadili ya Uchaguzi katika kuwasilisha malalamiko yao ya ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi, kwa mujibu wa sehemu ya 5.7(e) ya Maadili ya Uchaguzi, pale ambapo Chama cha Siasa au Mgombea hakuridhika na maamuzi ya Kamati ya Rufaa atakuwa na fursa ya kuwasilisha malamiko yake Mahakamani baada ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292”.

Amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kuwasihi viongozi wa Vyama vya Siasa na Wadau wengine wa Uchaguzi kuendelea na Kampeni za kistaarabu na kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi na kwamba inaendelea kufuatilia kwa karibu kila hatua ya Uchaguzi na hasa Kampeni huku akisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayekiuka Sheria za Uchaguzi.