Trending News

CCM Adverts and Promo

Friday, January 13, 2017

NEC YATOA UFAFANUZI WA MALALAMIKO YA UKIUKWAJI WA MAADILI YA UCHAGUZI YALIYOTOLEWA NA ACT-WAZALENDO.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima akitoa Ufafanuzi kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi yaliyotolewa na Chama cha ACT WAZALENDO

13/1/2017. Dar es Salaam.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekishauri Chama cha ACT – Wazalendo na Vyama vingine vyenye wagombea wa Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Dimani na Udiwani katika Kata Ishirini (20) za Tanzania Bara ,kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi kwenye Kamati za Maadili zilizo katika maeneo yao.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Kailima Ramadhan amesema NEC imepata taarifa kupitia Vyombo mbalimbali juu ya malalamiko ya Chama Cha ACT-Wazalendo kuvilalamikia Vyombo vya Dola pamoja na Watendaji wa Umma kufanya vitendo vyenye muelekeo wa kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Bw. Kailima amesema taarifa ya Chama hicho iliyotolewa kwenye Vyombo vya Habari Januari, 12 2017, imeeleza kuwa Watendaji wa Halmashauri ya Geita waliwakusanya Wazee katika Kata ya Nkoma waje na Vitambulisho vyao vya kupigia Kura kwa lengo la kuwapatia huduma ya afya bure jambo linalolalamikiwa na ACT- Wazalendo kwa madai kwamba Watendaji hao wana lengo la kuwahadaa Wazee hao ili wakipigie Kura Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, amesema katika malalamiko yake Chama cha ACT Wazalendo kimeibua tuhuma za wananchi kupokwa kadi za kupigia Kura ili wasiweze kushiriki katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 22, 2017.
Mkurugenzi Kailima amesisitiza kuwa ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 mtu kumiliki kadi ya kupigia kura isiyokuwa yake.
“Natoa wito kwa wananchi wote kwamba, ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 mtu yeyote kumiliki kadi ya kupigia kura isiyokuwa yake”  Amesema.
Amefafanua kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa  kuzingatia sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi inavikumbusha Vyama vya Siasa kuwa iwapo vitakuwa na malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani viwasilishe malalamiko hayo kwenye Kamati ya Maadili ngazi ya Kata ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio linalolalamikiwa.
“ Sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi yayosainiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Serikali na Vyama Vya Siasa inaeleza wazi muda wa kuwasilisha malalamiko kwa kuvitaka vyama au wahusika wenye malalamiko yoyote  kuyawasilisha kwa maandishi kwenye Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya ngazi husika ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio” Amesisitiza Kailima.
Amesisitiza kuwa iwapo Chama cha Siasa au Mgombea hataridhika na maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Kata, kwa kuzingatia sehemu ya 5.7 (a) ya Maadili ya Uchaguzi anatakiwa awasilishe rufaa yake kwa Msimamzi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo ndani ya saa 24 tangu maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya kata kutolewa.
Aidha, Bw. Kailima amebainisha kuwa kama Chama cha Siasa hakikuridhika na maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo, bado kwa kuzingatia sehemu ya 5.7 (b) na (c) kinayo fursa ya kuwasilisha Rufaa yake katika Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa au ngazi ya Rufaa ambayo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“ Tunavishauri Vyama vya Siasa na Wagombea kuzingatia matakwa ya Maadili ya Uchaguzi katika kuwasilisha malalamiko yao ya ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi, kwa mujibu wa sehemu ya 5.7(e) ya Maadili ya Uchaguzi, pale ambapo Chama cha Siasa au Mgombea hakuridhika na maamuzi ya Kamati ya Rufaa atakuwa na fursa ya kuwasilisha malamiko yake Mahakamani baada ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292”.

Amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kuwasihi viongozi wa Vyama vya Siasa na Wadau wengine wa Uchaguzi kuendelea na Kampeni za kistaarabu na kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi na kwamba inaendelea kufuatilia kwa karibu kila hatua ya Uchaguzi na hasa Kampeni huku akisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayekiuka Sheria za Uchaguzi.

No comments:

Post a Comment