Trending News

CCM Adverts and Promo

Tuesday, March 15, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli awaagiza Wakuu wapya wa Mikoa kusimamia ulinzi na usalama

Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli 


Raymond Mushumbusi - Dar es salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa wote nchini kusimamia ulinzi na usalama katika mikoa wanayoiongoza ili kuhakikisha suala la amani linaendelea kuwepo na kudumishwa nchini na watu watafanya kazi kwa bidii na hatimaye wataweza kujipatia maendeleo ya hali juu .

Akitoa agizo hilo mara baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli amesema suala la ulinzi na usalama wa mikoa lipo chini ya mkuu wa mkoa na hategemei kuona matatizo ya kiusalama yanashamiri katika mikoa wakati mkuu wa mkoa husika yupo.

“Nimewaamini na kuwapa nafasi za kuongoza mikoa, sasa basi naomba msimamie suala la ulinzi na usalama katika mikoa yenu sitegemei kuona kwa mfano wasafiri katika mikoa ya Kigoma au Kagera wanasindikizwa na polisi wakati wakisafiri hii itadhihirika wazi kabisa kuwa mkuu wa mkoa umeshindwa kazi,” alisema Rais  Magufuli.

“Kwanini Burundi au Rwanda hakuna majambazi lakini nchini kwetu ndani ya mikoa yetu vitendo vya ujambazi vimeshamiri, nawaagiza mkafanye kazi na wala msiogope mtu, tukawatumikie wananchi wetu kwani wanatutegemea,” alisema Rais Mhe.Dkt Magufuli.

 Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga amesema atatumia uzoefu alionao wa miaka 37 katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais  katika kusimamia masuala ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wa mkoa huo ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi na mali zao.

“Nitasimamia vizuri maagizo ya Mhe.Rais ya kusimamia suala la ulinzi na usalama katika mkoa wangu ukizingatia tunapakana na nchi kadhaa jirani ila nitafanya kazi niliyotumwa kuifanya ya kuwahakikishia wananchi wa Kigoma wanaishi na kufanya kazi zao za kila siku katika usalama,” alisema Brigedia Jenerali Maganga.

Rais Magufuli amewaapisha wakuu wa mikoa 25 kwenda kuwatumikia wanachi wa mikoa hiyo na kutatua changamoto katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta ya Afya,Elimu na Maji katika kuletea maendeleo pia amewaapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania(TRA) Alphayo Kidata na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna wa Polisi Valentino Longino Mlowola .




No comments:

Post a Comment