Trending News

CCM Adverts and Promo

Tuesday, April 19, 2016

SERIKALI YATOA AGIZO KWA SHULE BINAFSI

 Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof.Joyce Ndalichako.

WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imeziagiza shule zote za binafsi kuwa na mihula miwili tu ya masomo kwa mwaka badala ya kuwa na mihula mitatu au minne kama ilivyo kwa sasa katika shule hizo.

Agizo hilo liko kwenye Waraka wa Elimu Namba Moja wa Mwaka 2015, ambao unaeleza kuwa kuanzia sasa mihula ya masomo, itakuwa miwili kwa kila mwaka wa masomo kwa shule zote za serikali na zisizo za Serikali.

Waraka huo uliosainiwa na Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa umefafanua kuwa kila muhula, utakuwa na likizo fupi na likizo ya mwisho wa muhula. Siku za masomo kwa mwaka zitakuwa ni 194.

Waraka huo pia umeagiza wanafunzi wote, wapumzike mwezi Juni na Desemba na mashindano ya michezo ya shule za msingi (Umitashumta) na michezo ya sekondari (Umiseta), ifanyike mwezi Juni wakati wa likizo.
Kutokana na agizo hilo, wamiliki wa shule zisizo za serikali wametakiwa kuwasilisha wizara ya elimu kalenda za mihula ya masomo. Nakala ya waraka huo wamesambaziwa wakaguzi wote wa shule, walioko kwenye kanda na wilaya kuhakikisha wanazifuatilia shule zote ili ziweze kutii agizo hilo la Serikali.

No comments:

Post a Comment