Jumla ya wadaiwa wapya 21,721
wa mikopo ya elimu ya juu wamejitokeza ili kuanza kulipa madeni yao kufuatia
agizo la siku 60 lililotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) mnamo Machi 14 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi
wa Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
Bw. Robert Kibona wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu
tathmini ya agizo lililotolewa na bodi
hiyo kwa wanufaika wa mikopo na waajiri ili kutimiza wajibu wao kisheria.
Bw. Kibona alifafanua kuwa
jumla ya Shilingi bilioni 151.5 zinatarajiwa kurejeshwa na wadaiwa hao ambao
walikopeshwa ili kuwawezesha kupata elimu yao ya juu katika vyuo mbalimbali
ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 1994.
“Lengo la agizo lilikuwa ni kuhahakisha madeni yote
yaliyoiva yanakusanywa ili kuongeza uwezo wa kukopesha watanzania wengi zaidi
na agizo hili limeisha Mei 13 mwaka huu.” alisema Bw. Kibona.
Kwa mujibu wa Bw. Kibona, kati ya wadaiwa
waliopatikana, wadaiwa 19,528 walipatikana baada ya Bodi kuchambua taarifa za
waajiriwa zilizowasilishwa na waajiiri na wadaiwa wengine wapatao 2,007
walijitokeza kwa hiari.
“Waajiri wana wajibu wa kisheria wa kuwasilisha
taarifa za waajiriwa wao, baadhi yao walifanya hivyo katika siku hizo sitini na
tukawabaini wadaiwa hao, tunawapongeza waajiri kwa ushirikiano walioutoa na
wanufaika wote waliojitokeza kwa hiari” alisema Bw. Kibona.
Aidha Bw. Kibona aliongeza kuwa Bodi imeongeza
siku 30 za ziada kuanzia Mei 20, 2016 kwa wadaiwa waliobaki kujitokeza na
uamuzi huo umetokana na tathmini iliyoonyesha kuwa kuna idadi kubwa ya waajiri
na wanufaika wanaoendelea kujitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo Bw. Cosmas Mwaisobwa
alisema kuwa kiwango cha ukusanyaji wa madeni kwa mwezi kinatarajiwa kuongezeka
kutoka shilingi bilioni 2.7 zinazokusanywa hivi sasa na kufikia shilingi
bilioni 8 ifikapo mwezi Juni 2016.
Katika kipindi cha
mwaka 1994/1995 hadi sasa, kiasi cha shilingi trilioni 2.44 kimetolewa kwa
wanufaika 378,504 wakiwemo wanafunzi wanaoendelea na masomo yao hivi sasa ambao
kwa sasa hawana wajibu wa kulipa hadi pale watakapomaliza au kusitisha masomo
yao.
No comments:
Post a Comment