Na: Lilian Lundo - Dodoma
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewatoa wasiwasi watanzania juu
ya kodi ya ushuru wa bidhaa katika miamala ya benki na simu za mkononi kwamba
haitawaathiri wao ila makampuni ya simu.
Mhe.
Mpango ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akitolea ufafanuzi taarifa za
upotoshaji zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu namna Serikali
itakavyotekeleza Bajeti ya mwaka 2016/2017 iliyopitiswa jana na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa
sasa sheria inatamka kwamba ada itatozwa katika kutuma fedha tu, hata hivyo
baadhi ya kampuni za simu na benki zimekuwa zikitumia mwanya wa sheria hiyo
kupunguza wigo wa kodi kwa kutoza ada wakati wa kupokea,” alisisitiza Mhe.
Mpango.
Mhe.
Mpango aliendelea kufafanua kuwa, kwa kuwa makampuni ya simu na benki yamekuwa
yakitoza ada wakati wa kupokea fedha huku serikali haiwatozi kodi kwa fedha
zinazopokewa, hivyo basi Serikali imeamua kutoza ushuru kwenye ada ya kutuma na
kupokea fedha au vyote kwa kadri itakavyotozwa.
Aidha
Mhe. Mpango alisisitiza kwa kusema kuwa ushuru huo utalipwa na benki na kampuni
ya simu na siyo mtumiaji au mpokeaji wa fedha katika miamala itakayofanyika.
Hivyo
basi Waziri Mpango ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA)
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BOT)
kuhakikisha kwamba tozo hiyo inaendana na uhalisia wa huduma inayotolewa kwa
kufanya ukaguzi wa miamala ya makampuni
ya simu kabla na baada ya tozo ili yasihamishie mzigo kwa mtumiaji wa
mwisho.
Kuhusu
suala la kulipa kodi Mhe. Mpango amewasisitiza wananchi kulipa kodi kama
inavyotakiwa ili Taifa liweze kujenga uwezo wa kujitegemea na kuwaletea
wananchi wake maendeleo ya kweli kwa kuwa hiyo ndio dhamira ya Serikali ya
Awamu ya Tano.
No comments:
Post a Comment