Na. Ismail Ngayonga - Dodoma.
SERIKALI kupitia Bodi ya Utalii
Nchini (TTB) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), katika mwaka
2016/17 imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 2.7 kwa ajili ya kuitangaza sekta ya
utalii ndani na nje ya nchi.
Akijibu swali la mbunge wa Viti
Maalum (CCM), Maria Kangoye, leo Bungeni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhandisi Ramo Makani alisema bajeti hiyo ni ongezeko la asilimia 14.7 za fedha
za Serikali zilizotengwa katika bajeti ya mwaka ya 2015/16.
Makani alisema Serikali itaendelea
kuboresha sekta ya utalii kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo na
vyanzo vingine vya mapato kama ilivyoanishwa katika mpango wa maendeleo wa
miaka mitano 2016/17- 2020/21.
Alisema Serikali pia imepanga
kuimarisha Chuo cha Utalii katika kampasi za Bustani iliyopo Dar es Salaam,
Temeke na Arusha ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi na umahiri wa wakufunzi,
kuboresha upatikanaji wa vifaa vya kufindishia na kuboresha miundombinu ya
kampasi hizo.
“Kuhusu uimarishaji wa miundombinu,
Wizara yangu imetenga jumla ya Tsh. Milioni 500 katika bajeti ya mwaka 2016/17
ili kukamilisha ujenzi wa jengo la Utalii katika Bustani ya Chuo cha Utalii
Tanzania” alisema Mhandisi Makani
Aidha Mhandisi Makani alisema kuwa
Chuo cha Utalii Tanzania kwa kushrikiana na Chuo cha Vancouver University cha
Canada kupitia mradi wa ISTEP uliopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia ya Ufundi kitaanzisha mafunzo ya Uongozi katika shahada kuanzia
mwezi septemba 2018.
Aidha Mhandisi Makani alisema
Serikali inaendelea kuelekeza nguvu katika vyuo vilivyopo kwa kuongeza idadi ya
wahitimu wa ngazi ya kati na baadaye wa ngazi ya shahada, ambapo kwa sasa Chuo
cha Utalii Tanzania kitaanza kuboresha utoaji wa mafunzo katika tansia za
ukarimu na Utalii katika ngazi ya shahada.
No comments:
Post a Comment