Na John Luhende
Idadi ya mauzo katika soko la hisa Dar es salaam yameshuka kwa asilimia 81 na kufikia shilingi bilioni 2.1 kutoka shilingi bilioni 11.3 kutokana na kushuka kwa ukubwa wa mtaji wa soko kutoka trilioni 24.6 mpaka kufika trilioni 23.2.
Akizungumza na waandishi wa habari Afisa Masoko Mwandamizi wa DSE Bi. Mary Kinabo amesema kuwa idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa zimeshuka kwa asilimia 69 sawa na milioni 1.68 kutoka milioni 5.3.
Aidha Bi. Kinabo ameongeza kuwa licha ya kushuka kwa idadi ya mauzo ukubwa wa mtaji wa makampuni ya ndani umepanda kwa asilimia 0.88 na kufikia trilioni 8.4 kutoka trilioni 8.3.
Akieleza taarifa hiyo kwa kina mbele ya wana habari Bi.Kinabo amesema kuwa benki ya CRDB imeongoza kwa asilimia 38.08 katika idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa na kufuatiwa na DSE ikiwa na asilimia 27.55 pamoja na benki ya NMB kwa asilimia 22.94.
Pamoja na hayo Bi. Kinabo ametangaza majina ya washindi wa shindano la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (DSE Scholar Investment Challenge 2016) ni Godfrey Pantaleo kutoka Chuo cha Biashara Arusha , mshindi wa pili ni Benson Humphrey wa Chuo Cha Kilimo Sokoine na wa tatu ni Frank Kigodi wa Chuo Kikuu Dodoma.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment