Mtendaji
Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dk. Bakari Jabiri akitoa ufafanuzi kwa
Waziri Ofisi
ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (kulia) kuhusu
kituo cha ufuatiliaji mifumo ya mawasiliano Serikalini, Ofisi za Wakala ya
Serikali Mtandao (e-GA) jijini Dar es salaam.
Na.Aron Msigwa – Dar es salaam.
Matumizi ya Teknolojia ya
Habari na mawasiliano (TEHAMA) katika uendeshaji wa shughuli za serikali ( e-Government)
katika miaka ya hivi karibuni yameendelea kukua kwa kasi na kupata nguvu katika
nchi mbalimbali duniani kutokana na mchango wake katika kufanikisha utoaji wa
taarifa na huduma kwa wananchi kwa haraka na gharama nafuu.
TEHAMA imegusa maisha ya kila siku ya wananchi na
kurahisisha mawasiliano muhimu katika shughuli zao kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kijamii.
Aidha, TEHAMA imekuwa mkombozi katika kurahisisha na kuimarisha sekta ya
biashara na fedha.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2014 kuhusu matumizi ya Mtandao
katika shughuli za Serikali ( 2014 UN e- Government Survey) kwa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa
matumizi ya TEHAMA kwenye shughuli za Serikali duniani kote yamefanikiwa sana
kuwasogeza wananchi karibu na Serikali.
Matumizi hayo yameongeza uwazi,
uwajibikaji,ufanisi na matokeo makubwa yanayozingatia muda katika nyanja
mbalimbali zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi. Miongoni mwa nchi
zinazofanya vizuri zaidi duniani katika matumizi hayo ni Jamhuri ya Korea
ambayo imetajwa kuwa nchi ya kwanza ikifuatiwa na Australia na Singapore.
Nchi nyingine zinazofuatia ni Ufaransa,
Japan, Marekani, Uingereza, New Zealand, Finland,Uholanzi, Uruguay, Ireland,
Australia, Canada, Norway,Sweden, Iceland, Urusi,India,China, Ujerumani,
Israel, Denmark, Luxemburg,Italia, Ubelgiji, Hispania, Chile,Bahrain, Estonia
na Austria.
Kwa mujibu wa Ripoti hiyo Tanzania ni miongoni mwa
nchi za Bara la Afrika zilizo katika kundi la kati katika matumizi ya Serikali Mtandao. Nchi
nyingine za Afrika ambazo ziko kwenye kundi hilo ni Tunisia, Mauritius, Misri,
Seychelles, Rwanda, Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Botswana, Namibia, Nigeria,
Angola, Zimbabwe, Ghana, Swaziland, Gabon, Algeria, Cape Verde na Cameroon.
Kama tunavyojua Tanzania sio kisiwa,
haiwezi kujitenga na mabadiliko haya. Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa
matumizi ya mtandao katika shughuli za Serikali yameokoa muda wa watu
kufuatilia huduma na taarifa kutoka eneo moja hadi jingine, yamepunguza gharama
na usumbufu waliokuwa wakiupata wananchi wakati wa kulipia huduma na tozo mbalimbali za Serikali, utafutaji wa
taarifa za huduma, matangazo ya serikali na nafasi za ajira ambazo sasa
zinapatikana kwa njia ya mtandao.
Jukumu na
mamlaka ya kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini liko
chini ya Wakala ya Serikali Mtandao (e-Government Agency) iliyoanzishwa Aprili,
2012 chini Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1977.
Wakala hiyo pamoja na mambo mengine ilianzishwa kwa
lengo la kuboresha uwezo wa taasisi za umma kutekeleza jitihada za Serikali
Mtandao, kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo kwa umma, kuboresha mifumo
shirikishi ya TEHAMA, kusimamia uzingatiaji wa viwango pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam na msaada
wa kiufundi na huduma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt. Jabiri Bakari
anaifafanua dhana ya Serikali Mtandao kuwa ni matumizi ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA) katika taasisi za umma kwa lengo la kuboresha utoaji wa
huduma na taarifa kwa umma, kwa haraka na kwa gharama nafuu.
Anasema utekelezaji Serikali Mtandao umegawanyika
katika maeneo makuu manne ambayo ni kati ya Serikali na watumishi wake,
Serikali na Sekta ya Biashara, Serikali na Wananchi pia ni kati ya Taasisi moja
na Taasisi nyingine za Serikali.
Dkt. Jabiri anaeleza kuwa lengo la kuanzishwa kwa
Serikali mtandao nchini Tanzania ni kuimarisha utawala bora, kuongeza tija na
ufanisi katika uendeshaji wa taasisi za umma na kuhakikisha kunakuwa na
mawasiliano ya haraka yenye uhakika na salama ndani ya serikali na taasisi
zake.
Aidha, Serikali mtandao inapanua wigo wa
upatikanaji wa taarifa muhimu katika kila ngazi ya Serikali, kuimarisha usalama
wa serikali na raia wake pamoja na kuongeza uwezo wa Serikali kupambana na
majanga kwa kutumia teknolojia.
Anabainisha kwamba serikali mtandao inafanya kazi kama
ilivyo Serikali ya kawaida kwa maana ya mfumo (system) ambao ndani yake
una mifumo midogo midogo kwa maana ya taasisi mbalimbali, wakala, mashirika
na halmashauri ambazo zote hutengeneza
mfumo mkubwa mmoja wenye lengo la kuwahudumia wananchi.
Jambo linaloitofautisha Serikali mtandao na Serikali
ya kawaida ni suala la matumizi ya muda mchache katika kutoa huduma mbalimbali
kwa wananchi.Kupitia serikali mtandao mwananchi hujaza fomu kwa njia ya mtandao
kisha mifumo ya TEHAMA iliyowekwa huwasiliana na kubadilishana taarifa na kutoa
huduma stahiki kwa mwananchi.
Utendaji wa serikali unaotumia mfumo wa
mafaili/majalada ya kawaida (files system) hutumia muda mwingi
kushughulikia jambo moja, mwananchi anapoomba huduma anatakiwa kwenda kuchukua fomu kwenye ofisi
ya Serikali na kuijaza kisha kuiwasilisha moja kwa moja kwenye taasisi husika.
Mfano, mwananchi anapoomba Hati ya kusafiria kutoka
Serikalini, analazimika kwenda Idara ya Uhamiaji na kujaza fomu za maombi ya huduma. Hatua ya kujaza na kurejesha fomu hizo haichukui
muda mrefu isipokuwa pale tu inapoanza hatua ya uhakiki na utambuzi wa taarifa
zilizowasilishwa na mwananchi ili ziweze kufanyiwa kazi na taasisi husika.
Ni ukweli usiopingika kuwa zoezi la uhakiki wa taarifa
za mwanachi anayeomba Hati ya kusafiria au leseni ya udereva au kitambulisho
cha Taifa kwa njia ya kawaida bila kutumia mtandao huchukua muda mrefu kwa kuwa
suala la uhakiki wa taarifa zikiwemo za mwenendo wa makosa mbalimbali, kuzaliwa
na mambo mengine hufanywa na taasisi zaidi ya 4 au 5 wakati kupitia TEHAMA
jambo hilo lingeweza kufanywa ndani ya
siku moja.
Dkt. Jabiri anasema ili Serikali mtandao iweze fanya
kazi yake ipasavyo hapa nchini lazima kuwe
na miundombinu ndani au nje ya taasisi pia uwepo wa mifumo Tumizi ( Application Systems)
inayoshughulikia masuala mbalimbali, uwepo wa wafanyakazi uwepo wa Sera,
miongozo na taratibu za kusimamia TEHAMA
kuwezesha utoaji wa huduma mtandao (e - Services).
Dkt. Jabiri anasisitiza kuwa Tanzania iko kwenye hatua ya
kwanza na ya pili kwa kuwa taasisi za Serikali zipatazo 200 zina miundombinu na
tovuti zenye taarifa za awali za kumsaidia mtu kujua huduma inayotolewa na
taasisi husika ili aweze kuchukua hatua ya kupata huduma.
Katika hilo Wakala ya Serikali
mtandao imefanikiwa kusanifu Tovuti Kuu
ya Takwimu Huria (Open Data Portal) ambayo ina taarifa mbalimbali za
sekta tatu zilizopewa kipaumbele Maji,
Elimu na Afya.
Pia serikali ilianzisha Tovuti ya Ajira (Ajira Portal) kwa
lengo la kuwapatia wananchi taarifa za ajira serikalini, Tovuti Kuu ya
Serikali,Tovuti Rasmi ya Wananchi ambayo inamwezesha mwananchi kuwasilisha
maswali na hoja ambazo hujibiwa na
Serikali pamoja na uanzishaji mfumo wa Barua Serikalini (GMS) ambao sasa
unatumiwa na taasisi 117 za Serikali na Balozi za Tanzania ambao umejikita
katika kuimarisha mawasiliano kwa njia ya barua pepe na kuongeza usalama wa
ubadilishanaji taarifa.
Mtendaji huyo anaeleza kuwa katika awamu ya kwanza taasisi
75 za serikali na Wizara zote za Serikali kupitia mkongo wa taifa, pia Wakala
imeziunganisha Taasisi 72 zilizounganishwa kwa simu zinazotumia itifaki ya
Intaneti kwenye mkongo wa taifa ili kurahisisha mawasiliano na kupunguza
gharama.
Aidha, anaeleza kuwa suala la baadhi ya Taasisi za serikali kukawia kuunganishwa
kwenye mtandao huo linatokana na mapungufu yaliyokuwa kwenye miongozo na
taratibu zinazosimamia shughuli zaTEHAMA ikiwemo uanzishaji wa tovuti, jambo
ambalo Wakala hiyo inalisimamia sasa kwa kuzitaka taasisi zote za Serikali ziwe
na tovuti zenye mfumo unaofanana.
Anasisitiza kuwa licha ya mabadiliko ya kiutendaji
yanayotokea kwenye taasisi za Serikali, Wakala ya Serikali mtandao imekuwa
makini kuhakikisha hakuna mfumo unaoinuka dhidi ya mfumo mwingine lengo likiwa
kumhakikishia mwananchi huduma katika eneo moja kwa muda mfupi.
Meneja Habari,Elimu na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali
Mtandao Bi. Suzan Mshakangoto anasema kuwa katika kuimarisha matumizi ya
Serikali Mtandao nchini matumizi ya
mitandao isiyo rasmi katika shughuli za serikali kwa sasa hayana nafasi.
Anasisitiza kwamba mkakati uliopo ni kuhakikisha
mawasiliano na matumizi ya barua pepe nje ya mfumo wa serikali kwenye ofisi za
umma yanafungwa kabisa ili dhana ya Serikali mtandao ichukue nafasi yake.
"Mpaka sasa tumetoa mafunzo ya usimamizi na ujenzi wa
mtandao wa Mawasiliano serikalini na usalama wa Mtandao kwa kwa taasisi za
umma149 wakiwemo maofisa TEHAMA 226, mafunzo ya vituo vya uendeshaji wa vituo
vya Data kwa taasisi za umma 91 na mafisa TEHAMA 162 pamoja na mafunzo ya
usimamizi wa mfumo wa Barua Pepe Serikalini kwa taasisi 157" Anaeleza
Bi.Suzan.
Aidha, anaeleza kuwa mpaka sasa taasisi 200 za umma zina
tovuti ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma kwa wananchi.
Changamoto iliyopo ni Tovuti nyingi kukosa taarifa zilizohuishwa pia
kuunganisha maeneo ambayo bado hayajafikiwa hasa Halmashauri na vijiji ili
kuwezesha taarifa mbalimbali kupatikana kwa wakati.
Anafafanua kuwa hatua ya mifumo ya serikali kuchelewa
kufanya kazi pamoja katika kubadilishana taarifa linatokana na kwamba awali
hakukuwa na mfumo uliowezesha jambo hilo kufanyika kutokana na mapungufu
yaliyojitokeza kwenye Sera, miongozo na taratibu zinazosimamia masuala ya
TEHAMA nchini lakini sasa kuna mwongozo uliotolewa kuhakikisha mifumo ya
taasisi za Serikali inawasiliana na kufanya
kazi pamoja ili kuondoa mapungufu
yaliyokuwepo.
Kwa mujibu wa Bi. Mshakangoto, taasisi zaidi ya 72 za
serikali zikiwemo Wizara zote, Wakala, Bunge na Mahakama zimeunganishwa huku
halmashauri zilizounganishwa kwenye mkongo wa taifa zikifikia 77. Aidha kazi ya
kuzifikia halmashauri zilizobaki inaendelea ili kuwezesha mawasiliano ya
serikali kupita kwenye mkongo wa taifa.
Pia katika kuhakikisha kuwa huduma za Serikali zinamfikia
mwananchi kupitia simu za mkononi umeanzishwa mfumo shirikishi unaowarahisishia
wananchi kupata huduma za Serikali popote walipo. Mfumo huu uliobeba huduma
mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma unapatikana kupitia namba maalumu ya kutolea huduma
*152*00#, unaokoa muda wa kufuata huduma kwenye ofisi husika, unaondoa urasimu
na kupunguza mianya ya rushwa.
Matumizi ya serikali mtandao yataongeza ufanisi na tija
katika Taifa kwani upotevu wa muda na umbali vitapunguzwa kwa kiwango kikubwa
kama si kuondolewa kabisa. Hivyo watumishi wa serikali na wananchi kwa ujumla
tuitumie hii mifumo kwa ajili ya kuharakisha maendeleo.

No comments:
Post a Comment