Na. Aron Msigwa – NEC, Musoma
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kutekeleza programu endelevu za
kutoa elimu ya mpiga kura ili kuwaelimisha wananchi waliofikisha umri wa kupiga
kura kutekeleza wajibu na haki waliyonayo kikatiba ya kupiga kura katika chaguzi
zijazo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima
Ramadhani wakati akizungumza na waandishi wa Habari mjini Musoma kuhusu mkakati
wa NEC wa kuwafikia wananchi moja kwa moja kuwapatia elimu ya mpiga kura.
Amesema kuwa Tume hiyo imeanza kutoa elimu hiyo kwa kushiriki maonesho
na mikutano mbalimbali ukiwemo mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania
(ALAT) unaofanyika mjini Musoma kuanzia
Septemba 22 hadi 24 mwaka huu.
“Tumeamua kushiriki kwenye mkutano huu kwa kuwa hawa ni watendaji wa
Serikali katika ngazi za mitaa, tumekuja kutoa elimu ya mpigakura kwani suala
la elimu tunalipa kipaumbele” Amesema Bw. Kailima.
Amesema Tume imeandaa programu ya
kuwafikia wapiga kura moja kwa moja kwa kuweka mkakati wa kuhudhuria mikutano
yote ambayo iko kihalali ikijumuisha ile ya Mawaziri na Naibu Mawaziri , Makatibu
Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya.
Aidha, amefafanua kuwa Tume imemwomba Katibu Mkuu TAMISEMI ratiba ya
vikao vya Mabaraza ya madiwani ya halmashauri zote nchini kwa lengo la
kuwezesha wataalam wa Tume hiyo kutoa elimu ya Mpiga kura.
“Tumemwomba Katibu Mkuu TAMISEMI atusaidie kuweka ajenda ya kudumu kuhusu
utaratibu mzima wa uendeshaji wa uchaguzi na uelimishaji wa mpiga kura kwenye
vikao vya mabaraza ya Madiwani ambapo maafisa wa Tume walio katika ngazi za
halmashauri watapata fursa ya kutoa elimu ya mpiga kura katika vikao hivyo”
Amesisitiza.
Ameeleza kuwa NEC imejipanga kupanua wigo wa utoaji wa habari kupitia
vyombo vya habari hasa Televisheni,Redio, Magazeti na Mitandao ya kijamii ili kuwawezesha
wananchi wengi kupata elimu ya mpiga kura na taarifa sahihi kuhusu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi na majukumu yake.
“Tumejipanga kutumia vyombo vya habari, kila wiki tutakuwa na taarifa
na mada fupifupi zinazohusu mchakato mzima wa uchaguzi kwa maana ya uandikishaji
na zoezi zima la upigaji kura kujenga uelewa kwa jamii nzima kuhusu Tume ya
Taifa ya Uchaguzi” Amefafanua.
Amesema kuwa kifungu Na 4 (c) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 kinaelezea
wazi kuwa pamoja na mambo mengine Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina jukumu kutoa
elimu ya Mpiga kura, kuratibu Taasisi na
watu wenye uwezo wa kutoa elimu ya mpiga kura ili kuongeza uelewa miongoni mwa
jamii.
“Tunategemea kuanzia mwanzoni mwa mwezi Oktoba tutatoa tangazo la
kuzialika Asasi na taasisi zinazotaka kutoa elimu ya mpiga kura ziwasilishe
maombi yao Tume ya Uchaguzi pamoja na zana zao za kutolea elimu ili tuweze
kuwapatia kibali cha miezi 6 na baadaye tutafanya tathmini juu ya ufanisi wa
kazi wanayoifanya” Amebainisha Bw. Kailima.
Amesema lengo la kuzishirikisha taasisi na Asasi hizo ni kuondoa ombwe
lililokuwa linaonekana la utoaji wa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi
pekee kwa kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kila wakati ili kuongeza uelewa wa
wananchi katika chaguzi zijazo.
Aidha, amesema NEC imeandaa mpango mpya wa kuzifikia shule mbalimbali
za Sekondari hapa nchini utakaowawezesha wanafunzi wa shule zitakazochaguliwa
kuwa na Klabu za elimu ya mpiga kura.
Amesema programu hiyo itaiwezesha Tume kuwaelimisha wanafunzi waliofikisha umri wa kupiga kura na wale ambao
bado hawajafikia umri huo ili kujenga uelewa wao kuhusu elimu ya Mpiga kura.
“Tumeanza program hii kwa kuzitembelea shule mbili za Sekondari za
Isange (wasichana) na Shule ya Ufundi Musoma zilizo katika Manispaa ya Musoma,
tutaongea na wanafunzi ambao wamefikia
umri wa kupiga kura lakini bado hawajajiandikisha kupiga kura na wale ambao bado
hawajafikisha umri wa kupiga kura, tumenalenga kuanzisha klabu ya Elimu ya
mpiga kura kwenye shule moja katika kila wilaya ya Tanzania” Amesema.
Amefafanua kuwa kuanzishwa kwa klabu hizo kutawawezesha wanafunzi
kujadiliana kwa kina kuhusu mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura kwa mujibu wa
sheria iliyopo ili kufikia lengo la kuwa na shule moja yenye Klabu ya elimu ya
mpiga kura katika kila wilaya ifikapo
Januari 2020.
No comments:
Post a Comment