Afisa Uchaguzi wa NEC Bw. Stephen Elisante akiwaonyesha wanafunzi wa shule ya Sekondari Kidinda fomu maalumu zinazotumika kujaza matokeo ya uchaguzi katika vituo vya kupigia kura wakati akitoa elimu ya Mpiga Kurra kwa wanafunzi wa shule hiyo, Bariadi mkoani Simiyu.
Mwanasheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),Bi. Fausta Mahenge akitoa elimu ya mpiga kura kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria yanayosimamia chaguzi za Tanzania kwa wanafunzi 743 wa Shule ya Sekondari Kidinda wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Afisa Uchaguzi wa NEC Bw. Stephen Elisante akisisitiza
jambo kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Kidinda wakati akitoa elimu ya Mpiga
Kurra kwa wanafunzi wa shule hiyo, Bariadi mkoani Simiyu.
Makamu Mkuu wa Shule
ya Sekondari Kidinda Mwalimu Paul Susu akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo
mara baada ya kuwakaribisha Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi waliofika
shuleni hapo kutoa Elimu ya Mpiga Kura kwa wanafunzi wapatao 743 wa shule hiyo.
Mwanasheria wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC),Bi. Fausta Mahenge akiwaonesha mfano wa karatasi
inayotumika kupigia kura yenye majina ya wagombea wa vyama mbalimbali wakati
akitoa elimu ya Mpiga Kura katika Shule ya Sekondari Kidinda wilayani Bariadi
mkoani Simiyu.
Mwanafunzi wa Kidato
cha tatu wa shule ya Sekondari Kidinda, Filipo Madeni akiwauliza swali Maofisa
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu mfumo unaotumika kuwapata wagombea Urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wanafunzi wa shule ya
Sekondari Kidinda wakifuatilia kwa makini darasa la Elimu ya Mpiga kura kutoka
kwa maofisa wa NEC walioitembelea shule hiyo.
Na.Aron Msigwa – NEC,
Bariadi-SIMIYU.
Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) imetoa wito kwa wanafunzi wa shule za Sekondari waliopatiwa
elimu ya Mpiga Kura katika maeneo mbalimbali nchini kuwa mabalozi wazuri wa kuifikisha
elimu waliyoipata kwa jamii inayowazunguka.
Wito huo umetolewa na
Mwanasheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bi. Fausta Mahenge wakati akitoa
elimu ya mpiga Kura na kuhusu masuala ya kisheria na utendaji wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Kidinda Bariadi mkoani
Simiyu.
Amewaeleza wanafunzi
hao kuwa NEC imezindua programu ya
kuwafikia wanafunzi wa Shule za Sekondari na vyuo Vikuu ambayo haikuwepo hapo
awali ili kuwafikia vijana wengi zaidi kwa kuzingatia nafasi ya vijana katika
kufikisha elimu hiyo katika ngazi ya familia, mitaa na vijiji.
“ Baada ya elimu hii
nawaomba muwe mabalozi wa elimu ya mpiga kura katika maeneo yenu, ninajua ninyi
mmetoka katika mitaa na vijiji mbalimbali, mkawe mabalozi wa kuelezea kazi za
Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika ngazi za familia zenu ili tusaidiane kufikisha
ujumbe na kuiwezesha Tanzania kusonga mbele” Amesisitiza Bi. Fausta.
Amesema tangu kumalizika
kwa uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka 2015, NEC imekuwa ikitekeleza programu endelevu za
kutoa elimu ya mpiga kura katika maeneo mbalimbali ili kuongeza uelewa kwa
wananchi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kufanikisha chaguzi mbalimbali
zinazofanyika na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2020.
Ili kufanikisha lengo
hilo Tume itashirikiana na Asasi mbalimbali za Kiraia ambazo zitapewa vibali
maalumu ili kutoa elimu ya mpiga kura katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa ufafanuzi wa
kuhusu maswali yaliyokuwa yakiulizwa na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo
kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mipaka yake na maamuzi ya kisheria yanayochukuliwa
na baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi amesema kuwa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweka wazi mamlaka ya Tume katika kusimamia
na kuratibu shughuli za chaguzi nchini za kidemokrasia hapa nchini.
Amesema kwa mujibu wa sheria NEC inaratibu na
kusimamia Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na kutangaza matokeo ya
ngazi hizo kwa upande wa Tanzania Bara na kufafanua kuwa chaguzi za viongozi wa
Serikali za mitaa zimeachwa chini ya Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
“Kwa upande wa
Serikali za Mitaa, Sheria haiipi mamlaka Tume ya kusimamia chaguzi hizo badala
yake uchaguzi wa Serikali za Mitaa uko chini ya Wizara inayohusika na Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeachiwa jukumu hilo” Amesema.
Kuhusu kubatilishwa
kwa matokeo ya uchaguzi amefafanua kuwa Mahakama inaweza kubatilisha matokeo ya
mgombea yoyote pale taratibu za uchaguzi zinapokiukwa pia mgombea aliyepitishwa
kwa nafasi husika kugundulika kuwa amekosa sifa hali inayosababisha matokeo
yake kubatilishwa na Mahakama.
Kwa upande wake Afisa
Uchaguzi wa NEC Bw. Stephen Elisante akielezea historia ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) amesema kuwa ilianzishwa mara baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama
vingi nchini mwaka 1993 na kuongeza kuwa kuwa Ibara ya 74 kifungu cha 6 cha
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza majukumu ya NEC ikiwemo
kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapigakura na kusimamia uendeshaji wa uchaguzi
Tanzania Bara.
Amewaeleza wanafunzi
hao kuwa NEC ina mamlaka ya kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maeneo
mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge kwa kuzingatia vigezo mbalimbali
vikiwemo vya idadi ya watu, hali ya kiuchumi ya eneo na ukubwa wa eneo husika.
Naye Afisa Habari wa
NEC Bi. Margareth Chambiri akitoa ufafanuzi kuhusu programu ya NEC ya kutoa
elimu ya mpiga kura amesema kuwa NEC itaendelea kuwafikishia elimu ya Mpiga
kura wananchi ili kuongeza uelewa wa wananchi na kuondoa baadhi ya dosari
zilizojitokeza kwenye chaguzi zilizopita kabla ya uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2020.
“Licha ya changamoto
mbalimbali za Kijiografia katika kuwafikia wananchi tungependa kuona idadi
kubwa ya vijana na wananchi wanajiandikisha
na kujitokeza kupiga kura, naomba vijana mshiriki kikamilifu katika
kuwaelimisha wananchi kwa kuwa hii ndio Demokrasia tunayoitaka Tanzania vijana
mliopata elimu leo muwe chachu kwa wenzenu ili tuongeze idadi ya wapiga kura na
wagombea katika miaka ijayo” Amesisitiza.
Kwa upande wao walimu
na wanafunzi wa shule hiyo wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya
kumalizika kwa program ya utoaji wa elimu ya mpiga kura katika shule hiyo
wameishukuru NEC kwa kuwapatia elimu wanafunzi hao.
Wamesema hatua ya NEC
kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo inaongeza uelewa kwa wanafunzi wa shule
hiyo katika somo la Siasa na kuwafanya wanafunzi hao kuwa raia na wapiga kura
wema.
Wameiomba Tume ya
Taifa ya Uchaguzi kuendelea kutoa elimu hiyo kwa vijana wengi zaidi ili
kuwawezesha kuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu sahihi ya Mpiga Kura katika
maeneo mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment