Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimwapisha Bw. Alphayo Kidata kuwa Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Na Raymond Mushumbusi- Dar es salaam.
Serikali kupitia Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya takribani Sh. billioni 12 kutoka kwa
wafanyabiashara ambao walikwepa kodi na kupewa muda wa siku 14 na Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kulipa kodi hizo kwenye
mamlaka hiyo.
Akitoa takwimu hizo
mara baada ya kuapishwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Alphayo Kidata amesema, kila Mtanzania ana jukumu la kulipa kodi kwa mujibu wa
sheria na sio kukwepa na amehaidi kulisimamia vizuri suala la ukusanyaji wa
mapato katika sehemu mbalimbali ili kuongeza mapato ambayo yatasaidia
kufanikisha maendeleo katika sekta mbalimbali.
“Tutajitahidi kwa
kila namna kuwaelimisha wananchi wetu ili wafahamu wajibu wao na umuhimu katika
kulipa kodi na sio kukwepa kulipa kodi na tunawaomba wananchi kila waendapo
kupata huduma yoyote ile iwe katika sekta binafsi au Serikalini basi anatakiwa aombe stakabadhi za manunuzi au
huduma ili tuweze kudhibiti upotevu wa kodi” alisema Kidata.
Kamishna aliongeza kwamba Kidata mamlaka hiyo ipo kwa
ajili ya kuwahudumia wananchi na kama
kuna suala lolote au tatizo kuhusu kodi kuna ofisi katika mikoa yote ikiwa ni
hatua ya kutatua shida zao na kama kuna mtumishi yoyote wa mamlaka hiyo atashindwa
kumuhudumia mwanachi inavyotakiwa basi taarifa zitolewa mara moja kupitia namba
zao zilizoko kwenye tovuti ya mamlaka hiyo, ambayo ni www.tra.go.tz ili
kuimarisha huduma zetu kwa wateja.
Aidha Kamishna Mkuu huyo
amesema kuwa watawachukulia hatua wale wote ambao hawatalipa au hawajalipa kodi
zao kwa kuwapeleka mahakamani kwa kukaidi kulipa kodi halali kwa mujibu wa Sheria.
Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria na ina mamlaka ya usimamizi wa
makusanyo ya Mapato Tanzania na kwa kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na ukwepaji
wa kodi uliotokana na sakata la upotevu wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam
hivyo kuikosesha mapato Serikali lakini jitihada thabiti zimefanywa na mamlaka
hiyo kukusanya madeni kutoka kwa wakwepa kodi na kuwafikisha mahakamani ambao
wamekaidi kulipa.

No comments:
Post a Comment