Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji
Muhandisi Mbogo Futakamba akibonyeza moja ya mashine inayoongoza pampu za
kusukuma Maji kwenda jijini Dar es salaam kutoka Mtambo wa kuzalisha Maji wa
Ruvu Chini wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya majaribio ya
mtambo huo mara baada kukamilika kwa
ujenzi wa bomba la kusafirisha maji lenye urefu wa kilometa 55.9.
Mkuu
wa Matengenezo wa Mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini Tumaini Ndosi
(aliyepanda juu) akitoa ufafanuzi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Muhandisi Mbogo Futakamba
kuhusu moja ya mita inayosoma kiwango cha ujazo wa maji yanayosafirishwa kutoka
kwenye Pampu za kusukumia maji.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji
Muhandisi Mbogo Futakamba (kulia) akizungumza jambo na Meneja wa Mtambo wa
kuzalisha maji wa Ruvu Chini, Emmanuel
Makusa (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO Muhandisi Cyprian Luhemeja
mara baada ya kukagua mitambo na pampu za kusukumia Maji za Mtambo wa Ruvu
Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.
Eneo
la ndani la Mtambo wa kuzalisha maji likiwa limekamilika mara baada ya kufungwa
pampu mpya zenye uwezo wa kusukuma maji Lita milioni 270 kwa siku kuja jijini
Dar es salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji
Muhandisi Mbogo Futakamba (katikati) akieleza namna wakazi wa jiji la Dar es
salaam na mkoa wa Pwani watakavyonufaika na huduma ya Maji mara baada
kukamilika kwa ujenzi wa bomba la kusafirishia Maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini
kuja jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na
Maji Taka (DAWASA) Muhandisi Archard Mutalemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa
DAWASCO Muhandisi Cyprian Luhemeja.
Sehemu
ya maungio ya Mabomba yanayoingiza maji ndani ya Mtambo huo kutoka mto Ruvu,
chini.
Afisa
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASCO) Muhandisi
Cyprian Luhemeja akitoa ufafanuzi kwa waandishi namna DAWASCO ilivyojipanga
kuwahudumia wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kwa kuwafikishia huduma ya Maji
Safi kufuatia kukamilika ujenzi wa bomba la Maji kutoka Mtambo wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.
Sehemu ya Maungio ya bomba kubwa la Maji kutoka Mtambo wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani kwenda jijini Dar es salaam ikiwa imekamilika eneo la Tegeta
Na. Mwandishi Wetu - Dar es salaam.
Hatimaye moja ya Pampu
kubwa katika mtambo wa kuzalisha Maji kwenye chanzo cha maji cha Ruvu Chini,
Bagamoyo mkoani Pwani imewashwa kwa majaribio kufuatia kukamilika kwa mradi wa ujenzi
wa bomba kubwa la kusafirishia maji lenye urefu wa kilometa 55.9 kutoka chanzo
hicho kwenda jijini Dar es salaam.
Majaribio hayo ni
sehemu ya awali ya kupitisha maji yenye msukumo mkubwa kwenye bomba hilo kuelekea
kwenye matenki makubwa ya kuhifadhia maji yaliyoko eneo la Chuo Kikuu Ardhi
jijini Dar es salaam.
Akizungumza mara
baada ya kuwasha Pampu hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Muhandisi
Mbogo Futakamaba amesema kuwa majaribio hayo ambayo yameonyesha mafanikio yatawawezesha
wakazi wa jiji hilo na maeneo ya mkoa wa Pwani kupata huduma ya uhakika ya Maji
kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.
Amesema mradi huo utakuwa
suluhisho la tatizo la maji la muda mrefu kwa kuwa kiwango cha maji kitakachozalishwa kwa
siku kitafikia lita milioni 270 ambazo zitaongezwa
kwenye msukumo wa lita milioni 182 zilizokuwa zikizalishwa hapo awali kabla ya
kukamilika kwa ujenzi wa bomba hilo.
“Hii ni faraja kwa
Serikali na wakazi wa jiji la Dar es salaam na mkoa wa Pwani, DAWASA imetimiza jukumu lake, sasa tutapata
lita Zaidi ya milioni 270 kwa siku haya ni mafanikio makubwa, kulingana na
mahitaji tuliyokuwa nayo tutahakikisha tunayasambaza maji haya ili kukidhi
mahitaji ya wananchi” Amesema Muhandisi Futakamba.
Muhandis Futakamba
amewataka wahandisi na watendaji wanaosimamia uendeshaji wa mitambo hiyo kuwa
mahili na makini katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha inafanya
kazi kwa ufanisi na kwa maslahi ya umma.
Ameiagiza DAWASA
na DAWASCO kuendelea kuwajengea uwezo kielimu Wahandisi wa ndani wanaohusika na
utunzaji wa miundombinu hiyo ili miradi ya maji wanayoisimamia iweze kudumu na kuwa
endelevu kupitia matengenezo na huduma mbalimbali watakazozifanya.
“Ninyi kama
wahandisi na wasimamizi wa miradi na mitambo hii mikubwa hakikisheni mnajenga uwezo wenu wa ndani ili muweze kuiendesha
na kuidhibiti mitambo hii pia kuwa na uelewa wa ndani wa mifumo yote
iliyotumiwa wakati wa uwekaji wake na mabadiliko ya teknolojia” Amesisitiza.
Pia amewataka
watendaji hao kuhakikisha kuwa wanatunza mitambo na miundombinu yote ya maji ili
iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wake
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) Muhandisi Archard
Mutalemwa akizungumza mara baada ya kukagua mitambo ya kuzalisha Maji ya Ruvu
Chini amesema kuwa kukamilika kwa bomba hilo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali
kupitia DAWASA za kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya maji Safi.
Amesema DAWASA
itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuhakikisha inaendeleza na kusimamia
miradi ya maji ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo na kuhakikisha inawawezesha
wakazi wa jiji la Dar es salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani yanapata huduma ya Maji
Safi kupitia miradi iliyo chini yake.
Naye Afisa
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASCO)
Muhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza mara baada ya kuwashwa kwa mtambo huo
amesema kuwa DAWASCO imejipanga kuhakikisha inawasambazia huduma ya maji wakazi
wengi zaidi wa jiji hilo ambao walikua na miundombinu lakini hawapati huduma
hiyo pamoja na kuunganisha wateja wapya kwa gharama nafuu.
“Naishukuru
Serikali kwa kuwezesha mafanikio haya sisi kama DAWASCO tumejipanga na
tutahakikisha maji yanayozalishwa yanawafikia wananchi, yapo maeneo mengi
yaliyokuwa na changamoto ya huduma hiyo hata yale ambayo yalikua yameunganishwa
tayari katikati ya jiji nay ale yaliyo pembezoni mwa jiji tutahakikisha
tutayafikia” Amesisitiza.
Akizungumzia hatua
zinazochukuliwa kudhibiti wa wizi wa maji amesema DAWASCO imeanzisha maeneo 25 (DMA)
ambayo yamefungwa mita kubwa katika wilaya za jiji hilo ili kuwawezesha Mameneja
wa Zoni husika kuweza kubaini wizi , upotevu wa maji, ubovu wa mita na tatizo
la usomaji na kisha kuchukua hatua kwa wale wanaobainika kuhujumu miundombinu
hiyo.
Aidha, amesema DAWASCO imeandaa mpango wa
kuziondoa mita zote ambazo zimefikia umri wa miaka 10 ifikapo mwezi Juni mwaka
huu.
Ikumbukwe kuwa mradi
wa ujenzi wa bomba kubwa la kusafirishia maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini wenye
urefu wa kilometa 55.9 umejengwa na Kampuni ya JBG Gauff Ingenieure kwa gharama
ya shilingi Bilioni 141 ambazo zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania.





No comments:
Post a Comment