Trending News

CCM Adverts and Promo

Wednesday, March 16, 2016

SERIKALI YAENDELEA KUPOKEA MAOMBI YA WAWEKEZAJI UMEME


Serikali ya Tanzania imeendelea kupokea maombi ya wawekezaji hususani katika miradi mbalimbali ya uzalishaji na usambazaji umeme.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekutana na kuzungumza na Ujumbe kutoka Kampuni ya NARI Group Corporation ambayo ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Gridi ya Taifa la China, ambao walimweleza Waziri kuwa, pamoja na madhumuni mengine, wana nia ya kuzalisha umeme.

Makamu Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, Bao Tianhua amemueleza Waziri Muhongo kuwa, Kampuni yake inao mtaji wa kutosha pamoja na teknolojia ya kisasa katika uzalishaji umeme. Aliongeza kuwa Kampuni ya NARI ina uzoefu mkubwa katika kutekeleza miradi ya umeme kwani ilianza kufanya kazi kutoka miaka ya 1960.

Akijibu swali la Waziri kuhusu kiwango cha umeme ambacho Kampuni yake imejipanga kuzalisha endapo itakubaliwa maombi yake, Tianhua amesema wamejipanga kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 300 hadi 400 kwa kuanzia.

Kuhusu nia ya Kampuni yake kuwekeza katika uzalishaji wa umeme nchini, Tianhua amesema kuwa wangependa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika mradi huo ambapo NARI watawezesha masuala yote ya kiuchumi katika mradi.

Vilevile, amesema kuwa lengo lao ni kuzalisha umeme kwa kutumia gesi kupitia teknolojia ijulikanayo kitaalam kama ‘combined cycle’.

Akitoa mwongozo kuhusu maombi yaliyowasilishwa, Profesa Muhongo amewataka wawekezaji hao kukutana na kuzungumza na TANESCO pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ili kujadili kwa kina kuhusu mapendekezo husika na kwamba, iwapo maombi yao yatakubaliwa, ndani ya kipindi cha mwezi mmoja (Aprili 15 mwaka huu), NARI wanatakiwa wawe wamethibitisha iwapo watafanya uwekezaji huo ama la.

“Muda tunaotoa kwa sasa si zaidi ya mwezi mmoja, hivyo ndani ya mwezi mmoja, iwapo maombi yenu yatakuwa yamekubaliwa, mtapaswa kuwa mmewasilisha jibu lenu.”

Aidha, Waziri Muhongo amewataka NARI kuwasilisha kwa TANESCO na EWURA mapendekezo mengine waliyowasilisha kwake kuhusu nia ya kuwekeza katika miradi ya umeme vijijini kwa kutumia teknolojia ya makontena maalumu pamoja na miradi ya umeme jua. Aliwataka kuzungumzia hayo katika kikao kilichopangwa kufanyika baina yao.


No comments:

Post a Comment