WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kufutwa mara moja
umiliki wa mashamba makubwa 11 yenye ukubwa wa ekari 7,700 kwenye
vijiji vya Kasharazi na Rwakalemera wilayani Ngara Kagera, ambayo hayana hati
na yametelekezwa.
Ametoa agizo hilo leo asubuhi (Jumatano, Machi 16,
2016) wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Kasulo na Rwakalemera katika
kata ya Kasulo wilayani Ngara akiwa njiani kuelekea mkoa wa Geita.
Waziri Mkuu alilazimika kufanya mkutano huo mapema
asubuhi baada ya kuamua kuitisha uongozi wa wilaya ya Ngara ufike kwenye
mkutano huo ili kujibu kero za wananchi waliosimamisha msafara wake jana wakati
akielekea Ngara mjini.
Uamuzi huo unafuatia hatua ya Waziri Mkuu kumwita kwenye
mkutano huo Afisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya, Bi. Betty Munuo ili aeleze
chanzo cha mgogoro wa ardhi katika vijiji hivyo.
Bi. Munuo ambaye amehamishiwa wilaya hiyo Agosti, mwaka
jana, alisema aliyakuta malalamiko hayo na amefanya uchambuzi wa majina
ya wamiliki wote wa mashamba na walikuwa wanapanga kuwapatia notisi ili
wajieleze.
Katika orodha yake, Bi. Munuo alitaja wamiliki 18 wa
mashamba makubwa lakini kati yao ni wamiliki saba tu ambao mashamba yao yana
hati lakini matatu ndiyo yameendelezwa na manne hayajaendelezwa.
Mashamba yaliyoendelezwa yanatumika kwa kilimo,
ufugaji na shule. Nayo yanamilikiwa na Dayosisi ya Rulenge (shamba na. 606
lenye ekari 161 liko Mbuba); Dario Zakaria (shamba na. 639 lenye ekari 282 liko
Nyakariba) na Masista wa Mt. Fransisco (shamba na. 234 lenye ekari 759 liko
Kasulo).
Mashamba manne yenye hati lakini yametelekezwa ambayo
yote yako kijiji cha Rwakalemera ni ya Abdallah Sadala na. 235 lenye ekari 521;
Mahsen Saidi shamba na. 333 lenye ekari 458; Mshengezi Nyambele shamba na. 746
lenye ekari 388 na Mushengezi Nyambele shamba na. 745 lenye ekari 497.
Akitangaza uamuzi wake, Waziri Mkuu aliwataja wamiliki wa
mashamba yasiyo na hati kuwa ni Bw. Joseph Rugumyamheto mwenye shamba na. 527
(ekari 505 liko Rwakalemera); Bw. Nicolaus Kidenke shamba halina namba na
ukubwa wake haujulikani; Bw. Gwasa Angas Sababili shamba na. 714 (ekari 236
liko Kasharazi); na Bw. Makumi Adili Rufyega (ekari 500 liko
Rwakalemera).
Wamiliki wengine ambao mashamba yao yapo kijiji cha
Rwakalemera ni Paulo Shikiri ekari 250; Frank Mukama Derila ekari 750; Godfrey
Kitanga ekari 800; Philemon Mpanju ekari 200; Issa Sama ekari 500; Hekizayo
Mtalitinya ekari 225 na Joel Nkinga ekari 1,250.
Waziri Mkuu aliagiza ifanyike sensa ili kubaini kama
wamiliki wa mashamba hayo yote ni Watanzania au la. "Haya yenye hati
nataka yafanyike mapitio ya hati zao na kubainisha ni namna gani walipatiwa
hati hizo. Nataka taarifa inifikie ofisini kwangu Dar es Salaam ifikapo tarehe
20 Machi, 2016," alisema.
Ili kukamilisha kazi hiyo, Waziri Mkuu ameagiza
kurejeshwa mara moja kwa aliyekuwa Afisa Ardhi wa Wilaya hiyo, Bw. Enock Mponzi
ambaye amehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ili aje asaidie uchunguzi wa
ugawaji wa maeneo hayo.
Alimtaka Mwenyekiti wa kijiji cha Rwakalemera, Bw. Brighton
Kemikimba aitishe mkutano wa kijiji kabla ya tarehe 31 Machi 2016 na abainishe
mashamba yote makubwa ambayo yanazidi ekari 50. Pia afuatilie kama yana kibali
cha Baraza la Madiwani.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameagiza kusimamishwa kazi kwa
aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Bw. Colnel Ngudungi na
kutaka arejeshwe wilayani humo kujibu tuhuma za kuhusika na upotevu wa fedha za
mauzo ya mbao kutoka kwenye msitu wa Rumasi, wilayani humo.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Adam
Swai ameagizwa kumwandikia barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga ili
atekeleze maagizo hayo na Bw. Ngudungi arejeshwe Ngara kujibu tuhuma hizo. Bw.
Ngudungi alihamishwa kwenda Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga,
Agosti 2015.
Akiwa njiani kuelekea Ngara jana mchana (Machi 15, 2016),
waziri Mkuu alisimamishwa katika kijiji cha Rwakalemera na wananchi wenye
mabango wakiomba kurejeshewa ardhi ya kijiji huku baadhi yao wakidai
wanatishiwa na bunduki pindi wakisogelea mashamba hayo makubwa.
Pia walidai kuuzwa kwa msitu wa Rumasi na mapato
kutojulikana yalipokwenda huku wakidai kuwa kijiji chao hakipati mapato yoyote
kutokana na minada ya ng’ombe inayofayika kijijini hapo wakati sharia inataka
asilimia 20 ya mapato ibakizwe kijijini.
No comments:
Post a Comment