WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi
watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa tuhuma za ubadhirifu,
rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Watumishi hao ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na
Ushirika, Bw. Mwita Mirumbe Waryuba pamoja na Afisa Maendeleo ya Jamii wa
Wilaya, Bw. Dioniz Mutayoba.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana usiku (Jumatano,
Machi 16, 2016) alipokuwa akizungumza na watumishi wa idara zote na taasisi
zilizomo kwenye wilaya ya Chato katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa
Mshikamano SACCOS wilayani humo.
Afisa Kilimo na Ushirika anadaiwa kuchangisha kiasi
cha sh. milioni 20 kutoka kwa watumishi wa Halmashauri hiyo kwa ajili ya
kuanzisha SACCOS tangu mwaka 2013 lakini hadi sasa SACCOS haijaanzishwa na wala
fedha hizo hazijarejeshwa. Fedha hizo zinadaiwa kuliwa na watumishi watatu
(majina yamehifadhiwa).
Aidha, Bw. Waryuba anadaiwa kutumia lugha chafu na
za vitisho kwa watumishi walio chini yake ikiwa ni pamoja na kuomba na kupokea
rushwa, na kunyanyasa na kudhalilisha kijinsia baadhi ya watumishi wa kike.
Inadaiwa pia Bw. Waryuba alikopa bila kufuata
taratibu za mikopo wilayani Chato ambapo alikopa sh. milioni 15 kutoka Mwambao
SACCOS na sh. milioni 15 nyingine kutoka Chato Teachers’ SACCOS tangu mwaka
2015 na tangu wakati huo hajazirejesha hali ambayo imeleta manung’uniko kutoka
kwa viongozi na wananchama wa SACCOS husika.
“Malalamiko ya watumishi na wananchi dhidi ya huyu
bwana yamefikishwa kwa Kaimu Mkurugenzi lakini hajachukua hatua kwa sababu ni
rafiki yake,” alisema Waziri Mkuu. Kaimu Mkurugenzi huyo ni Mhandisi Joel Baha
ambaye hakuwepo ukumbini hapo kwa sababu yuko kwenye ziara ya mafunzo huko
Japan.
Kwa upande wake,
Bw. Mutayoba ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo anadaiwa
kuzembea kusimamia mradi wa kufyatua matofali ya gharama nafuu (interlocking
bricks) zilizogawiwa kwa vikundi vinne vya vijana wa wilaya hiyo.
“Mwaka 2013 Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilitoa
mashine nne za kufyatulia matofali ya bei nafuu kwa ajili ya vikundi vinne vya
vijana wilayani Chato. Mashine hizo ziligawiwa kupitia kwa Afisa Maendeleo ya
Jamii wa wilaya, Bw. Dioniz Mutayoba na kila kikundi kilipewa sh. 500,000 ili
waanze kazi ya kufyatua matofali na kuyauza kwa bei nafuu katika maeneo
waliyopo lakini hadi leo hakuna kitu kilichofanyika,” inasema sehemu ya
taarifa.
Afisa huyo anadaiwa kugawa mashine mbili kwa kila
kata katika kata za Muganza na Buseresere lakini hadi sasa hakuna
kilichofanyika kwani vikundi hivyo havikuzalisha kitu chochote tangu wakati
huo.
Aidha, Bw. Mutayoba anatuhumiwa kudai na kupokea
rushwa kwa wanachama wa vikundi vya ujasiriamali ili aweze kuvisaidia kupata
mikopo. “Yaani watu wanakuja kukopa sh. milioni mbili halafu unawadai kitu
kidogo cha sh. 300,000. Sasa mradi waliotaka kufanya wataweza kuukamilisha
kweli?,” alihoji Waziri Mkuu.
“Huyu bwana amelalamikiwa lakini Mkurugenzi
aliyepita lakini naye anadaiwa kumlinda kwa sababu ni rafiki yake,” alisema
Waziri Mkuu na kuibua minong’ono ndani ya ukumbi huo. Aliyekuwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Chato, Bw. Clement Berege hivi sasa amehamishiwa Halmashauri ya
Wilaya ya Iramba.
“Katika Serikali hii tunataka tuwe na Halmashauri
zilizo safi. Lakini pia Serikali hii ina mkakati wa kuimarisha ushirika na
tunataka kuinua kilimo. Kwa hiyo basi, TAKUKURU na polisi wachunguzeni hawa watu
wawili kwa maana ya Afisa Ushirika na Afisa Maendeleo ya Jamii na nipewe
taarifa uchunguzi utakapokamilika,” alisema Waziri Mkuu.
Mapema,
akizungumza na watumishi hao, Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Geita kwa
ziara ya siku mbili akitokea mkoani Kagera, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha
watumishi hao wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali hali zao na
akasisitiza kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza wajibu
wake.
“Napenda kusisitiza kuwa malengo ya Serikali ni
kuimarisha utendaji wa watumishi lakini pia Serikali hii haitamvumilia mtu
mdanganyifu, mzembe, asiye mwadilifu na mla rushwa. Ukiharibu kazi hapa Chato
mwwisho wako ni hapa hapa tu. Usitarajie kupelekwa Bunda au kwingine ili
ukaharibu na huko,” aliongeza.

No comments:
Post a Comment