| Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Magufuli akisalimiana na baadhi ya viongozi mara baada ya kuwasili katika ufunguzi wa Daraja la Kigamboni leo |
| Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Magufuli akiwasalimia wananchi waliohudhuria halfa ya uzinduzi wa daraja la Kigambini leo |
| Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Magufuli akikata utepe ishara ya kulizindua rasmi daraja la Kigamboni |
| Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Magufuli pamoja na viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo wakifurahia kuzinduliwa kwa daraja la Kigamboni |
Na.Mwandishi Wetu - Dar- es -Salaam.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli amezindua rasmi daraja la Kigamboni lenye urefu wa mita 680 ambalo
limegharimu kiasi cha dola za kimarekani milioni 135.0.
Akizungumza katika
sherehe hizo leo jijini Dar es Salaam
Mhe.Dkt.Magufuli ameeleza kuwa fedha za mradi huo ni mapato ya ndani
ambapo serikali imechangia asilimia 40 huku asilimia 60 zikiwa zimetolewa na
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF.
Aidha aliongeza kuwa
kupitia daraja hilo kero zilizokuwa zikiwakumba wakazi wa Kigamboni na maeneo
ya jirani zitakuwa zimepungua kwa kiasi kikubwa na hivyo kuwapa unafuu katika
usafiri.
“Kukamilika kwa
daraja hili kwa kiasi kikubwa kumesaidia kuondoa kero waliokuwa wakikutana nazo
wakazi wa Kigamboni hususani pale kivuko kinapokuwa na hitilafu kwa sasa watakuwa na urahisi wa kupita na
kuweza kufika katika maeneo yao ya kazi mapema,”alisema Mhe.Dkt.Magufuli.
Aliongeza kuwa
Serikali inafanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa inatatua kero ya foleni katika
jiji la Dar es Salaam kwa kumaliza
tatizo hilo na ikishindikani kumaliza
basi ni kulipunguza.
Mhe.Dkt.Magufuli
alisema kupitia daraja hilo uchumi wa
wananchi wa Dar es Salaam na Tanzania
kwa ujumla utaongezeka kupitia wawekezaji ambao watawekeza katika
maeneo ya Kigamboni pamoja na utalii wa kulitembelea daraja hususani
nyakati za usiku ambapo huwa linavutia sana.
“Daraja hili ni
kivutio kikubwa cha utalii ukizingatia ni daraja la kwanza kujengwa katika nchi
za ukanda wa Afrika ya Mashariki na nyakati za usiku linakuwa na sura nzuri
kupitia taa zilizowekwa maeneo haya” alisema Mhe.Dkt. Magufuli.
Pia alitoa wito kwa
kuwaomba watanzania kuwa wazalendo kwa kulipa kodi ili serikali iweze kupata
fedha za kujenga miradi mingine mingi kwa manufaa ya wananchi na hivyo
kubadilisha maisha yao kupitia huduma mbalimbali.
Pia aliwasihi
wananchi kuwa watu wa kuthamini na kutunza miradi inayotekelezwa na serikali
kwa kulitunza na kulithamini daraja hilo huku kila mmoja akiwa mlinzi wa
mwenzake kwa kutoa taarifa katika mamlaka husika pale anapoona uharibifu
unatendeka .
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na
Mawasiliano Mhe.Eng.Edwin Ngonyani ameeleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa
daraja hilo ni maendeleo makubwa kwa Dar es Salaam na nchi ya Tanzania kwa ujumla
kwa kuwa utarahisisha hali ya usafiri kwa wakazi wa Kigamboni na hivyo kuvutia
wawekezaji zaidi.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Eng.Patrick Mfugale
amebainisha kuwa ujenzi wa daraja la Kigamboni ulianza kufanyiwa usanifu tangu
mwaka 1976 na 1978 lakini utekelezaji wake ulikuja kufanyika mwaka 2012 ambapo Rais mstaafu wa
awamu ya nne Mhe.Dkt.Jakaya Kikwete aliweka jiwe la msingi na hatimaye leo
limezinduliwa na Rais wa awamu ya Tano Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli.
Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Hifadhi ya Jamii Prof.Godius
Kahyarara ameeleza kuwa ujenzi wa Daraja la Kigamboni umekamilika chini ya
mkandarasi wa kampuni ya China Railway Construction Engineering Group ikishirikiana
na kampuni ya China Major Bridge Engineering.
Mapokezi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akiwasili Kigamboni kuzindua daraja hilo.
Baadhi ya wananchi na wageni mbalimbali waliohudhuria ufunguzi wa daraja hilo leo
Daraja la Kigamboni kama linavyoonekana mara baada ya kukamilika.Daraja hilo lina urefu wa mita 680.
Sehemu ya majengo ya Utawala na uendeshaji wa daraja hilo





No comments:
Post a Comment