SERIKALI kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
inashauriana na Wawekezaji wa Viwanda vinavyofanya kazi kwa kusuasua pamoja na
vile vilivyofungwa ili kuviwezesha kufanya kazi.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati akijibu swali la
Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Savelina Mwijage ambaye alitaka kujua Serikali ina
mpango gani wa kuviboresha viwanda vya kizamani ili viweze kufanya kazi vizuri
kwa faida ya nchi.
Mhe. Mwijage amesema kuwa, viwanda vingi vinavyotumia
teknolojia ya zamani ambavyo havifanyi kazi au kuzalisha kwa kusuasua ni vile
vilivyobinafsishwa ambapo katika tathmini iliyofanywa na Wizara hiyo kwa kushirikiana
na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaonyesha kuwa kati ya viwanda
vilivyobinafsishwa, viwanda 24 vinafanya kazi kwa kusuasua na viwanda 37
vimefungwa kote nchini.
Aidha, katika mkoa wa Kagera, Kiwanda cha NMC Old Rice Mill
kimefungwa wakati kiwanda cha Kagera Tea Co. Ltd (MARUKU) kinafanya kazi kwa
kusuasua.
“Kusuasua kwa kiwanda hiki na vingine vyote nchini kunatokana
na uchakavu wa mitambo katika baadhi ya Viwanda, ushindani katika soko,
kupungua kwa mtaji na kutopatikana kwa malighafi”, alisema Mhe, Mwijage.
Ameongeza kuwa, Serikali inafanya majadilaino na wawekezaji
wa viwanda vinavyofanya kazi kwa kusuasua pamoja na vile vilivyofungwa ili
kuviwezesha viwanda hivyo kufanya kazi tena ambapo katika majadiliano hayo
yanayoendelea, yanahimiza matumizi ya ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji
viwandani.
“Tunawashauri wawekezaji walioshindwa kuendesha ipasavyo
viwanda vyao kuingia ubia na wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuviendesha kwa
tija ili tuongeze ajira, tuzalishe bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na nje na
kulipa kodi”, alisema Mhe. Mwijage.
Amesisitiza kuwa, Wizara yake kwa kushirikiana na Mamlaka
nyingine itaendelea kulinda viwanda vya ndani kwa kuhakikisha bidhaa zote ziingiazo
zinakidhi viwango na zinatozwa tozo stahiki.
“Tutahakikisha kuwa tunaboresha wepesi wa kufanya biashara
kwa kuondoa tozo kero na kuhakikisha kuna umeme wa uhakika wakati wote”,
alisisitiza Mhe. Mwijage.

No comments:
Post a Comment