Na. Fatma Salum-
MAELEZO, Dodoma.
Serikali imewahakikishia
wananchi kuwa inaendelea na utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa zahanati kila
kijiji, vituo vya afya kila kata na Hospitali katika kila Wilaya ikiwa ni
mkakati wake wa kuboresha huduma za afya kote nchini.
Hayo yamesemwa leo
bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Suleiman Jafo wakati akijibu swali la Mbunge wa
Busokelo Mhe. Fredy Mwakibete kuhusu Mpango wa kujenga zahanati kila Kijiji na
kituo cha afya kila Kata.
Mhe. Jafo alisema
kuwa Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi inaendelea na ujenzi wa
zahanati, vituo vya afya na Hospitali kila Wilaya ambapo ujenzi huo unafanyika
chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM).
“Utekelezaji wa
Mpango huo unaendelea na kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri
zimetengewa shilingi bilioni 182.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya afya
na kipaumbele kitatolewa katika kukamilisha miradi viporo badala ya kuanzisha
miradi mpya.” alisema Jafo.
Kwa mujibu wa Mhe. Jafo, Ofisi ya Rais
TAMISEMI inafanya tathmini ya utekelezaji wa mpango wa MMAM ili kujua idadi ya
Vijiji ambavyo havina zahanati, Kata ambazo hazina vituo vya afya na Wilaya
ambazo hazina Hospitali lengo likiwa ni kuhakikisha maeneo hayo yanapewa
kipaumbele na kutengewa fedha ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Akieleza mafanikio ya
mpango wa MMAM, Mhe. Jafo alisema kuwa chini ya mpango huo vituo vya kutolea
huduma za afya vimeongezeka kutoka 5,255 mwaka 2006/2007 hadi 6,935 mwaka
2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 39.9 hivyo kuna matumaini makubwa ya kuvifikia
vijiji vingi kupitia mpango huo.
No comments:
Post a Comment