Na.Aron Msigwa - Dodoma
Serikali imesema kuwa inaendelea na utaratibu wa kuzitambua
na kuzirasimisha bandari Bubu zote zilizokidhi vigezo ambazo zinatumiwa na
wafanyabiashara kupitisha bidhaa mbalimbali ili ziweze kuchangia katika Pato la
Taifa kulingana na wingi wa bidhaa zinazopitishwa
katika bandari hizo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Edwin Ngonyani ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo wakati akijibu
maswali ya Wabunge waliotaka kujua mkakati wa Serikali katika kudhibiti bidhaa
zinazoingizwa nchini na wafanyabiashara wasio waaminifu kupitia bandari bubu
hali inayoikosesha serikali mapato.
Mhe. Ngonyani amekiri kuwepo kwa ongezeko la
wafanyabiashara wasio waaminifu wanaotumia bandari hizo katika maeneo
mbalimbali nchini hasa ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi, Ziwa Tanganyika,
Ziwa Victoria na maeneo ya mipakani ambayo yanaingia moja kwa moja kwenye
makazi ya watu akieleza kuwa wengi wa wafanyabiashara wanakwepa kodi na
kutafuta urahisi wa kupitisha mizigo yao.
Amesema maeneo hayo yamekuwa chanzo kikubwa cha upitishaji
wa bidhaa zisizokidhi viwango, Silaha na Biashara haramu na kubainisha kuwa
baadhi ya wafanyabiashara wa ndani wasio waaminifu wamekuwa wakishirikiana na
raia wa kigeni kuagiza na kuingiza bidhaa hizo kupitia bandari hizo kwa lengo
la kukwepa kodi.
Amesisitiza kuwa
Serikali ya Awamu ya tano inalishughulikia kwa nguvu zote suala hilo
kupitia watendaji wake wakiwemo wakuu wa mikoa wa maeneo husika ambao
hushirikiana na mamlaka zinazohusika vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti
njia na maeneo yote yanayotumiwa na wafanyabiashara hao.
" Kama Serikali tunaendelea kufanya vikao kwa
kushirikiana na wakuu wa mikoa na mamlaka zinazohusika kuangalia namna ya
kurasimisha bandari bubu zilizobaki ili tuweze kukusanya mapato ya Serikali
yaliyokuwa yakipotea kutokana na wingi wa mizigo inayopitishwa" Amesema
Mhandisi Ngonyani.
Amefafanua kuwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2015 na
mwezi Januari, 2016, doria zilizofanyika
katika maeneo yanayotumiwa na wafanyabishara hao zilifanikisha kukamatwa kwa
wafanyabiashara 98 ambao wote walichukuliwa hatua za kisheria ikiwem mali zao
kutaifishwa pamoja na kuwafikisha
mahakamani.
Kuhusu bandari bubu zilizotambuliwa na kuzirasimishwa na
Serikali katika Pwani ya Bahari ya Hindi
ni Mbweni ya jijini Dar es salaam,
Mlingotini mkoani Pwani, Kisiju na Nyamisati mkoa wa Pwani na Bandari bubu ya
Kilambo mkoani Mtwara.
Aidha, amesema Serikali inaendelea na utaratibu wa
kurasimisha bandari binafsi umefanyika katika ziwa Victoria mkoani Mwanza na
maeneo mengine ambayo serikali inaendelea kuyafanyia kazi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.
Hamad Masauni amesema kuwa Serikali
inaendelea kuvijengengea uwezo vikosi vyake vya ulinzi na usalama kwa
kuviongezea vifaa vya kisasa ili viweze kuimarisha doria nchi nzima ili
kukabiliana na vitendo vyote vya uvunjaji wa sheria.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na
wananchi kukusanya taarifa za kiharifu ili kuwabaini na kuwakamata
wafanyabishara wote wanaojihusisha na uagizaji na uingizaji wa bidhaa kupitia
bandari bubu ambaoumekua ukiisababishia
serikali ikose mapato.
" Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea
kukusanya taarifa za kiharifu kutoka kwa wananchi ili kukabiliana na wimbi
hili, pia tunaendelea kuviongezea nguvu vikosi vyetu vya ulinzi na usalama ili
viweze kutimiza majukumu yao ipasavyo" Amesisitiza Mhe.Masauni.
No comments:
Post a Comment