Na. Immaculate Makilika- Dar es salaam.
Serikali imesema iko
tayari kuboresha reli ya Mamlaka ya Reli ya
Tanzania na Zambia(TAZARA) ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi kwani ni jambo
la msingi na itashirikiana na nchi za Zambia na China ili kufanikisha azma
hiyo.
Akizungumza leo
jijini Dar es salaam Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi wakati akizindua kikao kazi kilicho
shirikisha nchi tatu ambazo ni Tanzania,
Zambia na China kuhusu maboresho ya kiutendaji ya reli ya TAZARA.
“Kipaumbele chetu ni kuboresha reli ya TAZARA ili iweze kufanya
kazi kwa ufanisi, kikao hiki kitajadili kwa kina changamoto mbalimbali zinazoikabili
reli hii, pamoja na fursa zilizopo na namna ya kutatua changamoto hizo ili
kufufua uchumi wetu kupitia reli ya TAZARA” amesema Balozi Kijazi.
Balozi Kijazi amesema kwa muda sasa reli hii imekua ikifanya
kazi bila ufanisi kutokana na sababu mbalimbali licha ya kuwa kiwango cha
mizigo kutoka bandari ya Dar es salaam kimeongezeka kutoka tani milioni 6 mwaka 2006 hadi kufikia tani milioni 15 mwaka
2015, reli ya TAZARA imeshindwa kuwa na uwezo
wa kusaidia kusafirisha mizigo hiyo, ambapo mwaka kila mwaka uwezo wake
unashuka kutoka kusafirisha mizigo tani 601,229 mwaka 2005/2006 hadi tani
87,860 kwa mawaka 2014/2015.
Vile vile, licha ya kuwa nchi za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeongeza
uzalishaji wa shaba bado TAZARA haikuwa
na uwezo wa kuhudumia ama kusafirisha shaba hiyo, utendaji huu wa kiwango cha
chini lazima ubadilike.
Aidha, Serikali imesema ina nia ya dhati ya kuibadilisha
Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati, na yenye viwanda, kwa kujua kuwa uanzishwaji
mzuri wa mtandao wa miundombinu hasa reli, barabara, usafiri wa anga, usafiri
wa majini ni chanzo muhimu ya kutimiza azma hiyo.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Mawaziri la Zambia Dkt.
Rowland Msiska amesema kuna haja kubwa ya kuboresha reli ya TAZARA kwa kuwa
reli hiyo ina msaada mkubwa kiuchumi si tu kwa nchi za Tanzania, Zambia na
China bali hata nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC) na nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.
Aidha, amesema kuna faida nyingi za kuboresha reli ya TAZARA
ikiwemo ya gharama nafuu. Usafirishaji mizigo kwa njia ya reli ni wa gharama
nafuu kuliko barabara kwani inagharimu senti 5 kwa tani moja kwa umbali wa
kilometa moja, huku gharama za usafirishaji kwa barabara ikiwa ni senti 12 kwa
tani moja kwa umbali wa kilometa moja.
Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Biashara ya China, Bwana.
Liu Junfeng amesema Serikali yake itaendelea
kushirikiana na nchi za Tanzania na Zambia ili kuboresha utendaji wa reli hiyo,
huku akisisitiza uhusiano wa nchi hizi tatu umeendelea kuimarika na unazalisha fursa nyingine za ushirikiano.
Reli ya TAZARA ilijengwa mwaka 1970 hadi 1976 kwa msaada wa
Jamhuri ya watu wa China kama zawadi kwa mataifa ya Tanzania na Zambia, kwa
lengo la kusaidiza kuongeza njia za usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment