Na Jacquiline Mrisho – Dar es salaam.
Manispaa ya Ilala kwa
kushirikiana na Shirika la Misaada la Korea (KOICA) inatarajia
kutumia kiasi cha shilingi bilioni 18 kukamilisha Ujenzi wa Hospitali ya kisasa
ya kutolea huduma za matibabu kwa mama na mtoto katika Kata ya Chanika,wilayani
Ilala.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Afisa Habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, David Langa wakati akitoa ufafanuzi kuhusu maboresho yanayofanywa katika Sekta ya Afya
ndani ya Manispaa hiyo.
Amesema hospitali hiyo itakamilika mwishoni mwa mwaka huu na kuongeza kuwa
itakuwa na vitanda 266 pamoja na mashine zote za upasuaji na matatibu ya magonjwa
yote ya wanawake na watoto.
“Ujenzi wa Hospitali hii
kubwa ya wanawake na watoto unaendelea, tutatumia shilingi bilioni 18 kukamilisha
kazi ya ujenzi na kuweka vifaa vya
kisasa”,amesema Langa.
Kwa upande wake Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dkt. Meshach Simwela amesema kuwa hospitali hiyo itakapokamilika
itakuwa na vifaa vya kisasa pamoja na madaktari bingwa kutoka hospitali ya Taifa
Muhimbili, Amana, Mnazi Mmoja pamoja na hospitali nyingine za Serikali.
“Mpaka sasa jumla ya
waganga watano na wauguzi sita wameshapelekwa Korea kujifunza namna ya kutoa
huduma na jinsi ya kutumia vifaa vipya vitakavyoletwa mara baada ya Hospitali
hii kukamilika”, alisema Simwela.
Ameongeza kuwa ujenzi
huo unategemewa kukamilika mwaka huu na unategemewa kufunguliwa na Rais wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli au Makamu wa Rais
Mhe.Mama Samia Suluhu kwa kuwa ni Hospitali ya kwanza nchini Tanzania kuwa na
hadhi kubwa kama hiyo.
No comments:
Post a Comment