Waandishi wa Habari
wakifatilia kwa makini maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za
Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Ephraim Kwesigabo hayupo pichani akitoa
taarifa ya mfumuko wa bei wa taifa wa mwezi Juni 2016 leo Jijini Dar es
salaam.
Habari/Picha Na Ally Daud - Dar es salaam.
Mfumuko
wa bei wa taifa wa mwezi Juni, 2016 umeongezeka hadi asilimia 5.5 kutoka
asilimia 5.2 mwezi uliopita kutokana na kuongezeka kwa kasi ya upandaji wa bei
za bidhaa na huduma.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu
za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephaim Kwesigabo amesema kuongezeka kwa
mfumuko wa bei kumesababishwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za
vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi.
“Mfumuko
wa bei umesababishwa na kuongezeka kwa bei za vyakula kama vile mahindi ambayo
yameongezeka kwa asilimia 3.2, unga wa muhogo kwa asilimia 2.4, samaki wabichi
kwa asilimia 3.8, maziwa mgando kwa asilimia 4.3, maharage mabichi yaliyomenywa
kwa asilimia 6.1, vitunguu swaumu kwa asilimia 12.5, njegere kwa asilimia 6.2,
viazi mviringo kwa asilimia 2.5, mihogo mibichi kwa asilimia 6.7, magimbi kwa
asilimia 4.5, na ndizi za kupika kwa asilimia 2.7,” amesema Kwesigabo.
Amesema
bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei ni pamoja
na huduma ya kinywa na meno ambayo imeongezeka kwa asilimia 13.8, mafuta ya
dizeli kwa asilimia 2.4 na mafuta ya petroli kwa asilimia 4.3.
Kwesigabo
amesema mfumuko wa bei wa mwezi Juni, 2016 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi
umeongezeka kwa asilimia 0.5 ongezeko sawa na mwezi uliopita.
Aidha
amesema mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwaka wa bidhaa za vyakula majumbani na
migahawani umeongezeka hadi asilimia 8.3 mwezi Juni, 2016 kutoka asilimia 7.2
mwezi Mei, 2016. Fahirisi za bei zimeongezeka hadi 103.47 mwezi Juni, 2016
kutoka 103.00 mwezi uliopita.
Kwesigabo
amesema uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma
umefikia Shilingi 96 na senti 65 mwezi Juni, 2016 kutoka mwezi Disemba, 2015.
|
No comments:
Post a Comment