Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Moses Kusiluka akiwaeleza
waandishi wa Habari kuhusu mpango wa Serikali wa kupima na kurasimisha maeneo
yasiyopimwa katika jiji la Dar es salaam leo.
Na. Aron Msigwa
– DAR ES
SALAAM.
Serikali kupitia Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa mpango maalumu wa upimaji wa
Ardhi na Urasimishaji wa maeneo yote yasiyopimwa katika jiji la Dar es salaam
ambapo viwanja zaidi ya laki tatu
(300,000) vitapimwa na wamiliki wake kupewa Hati.
Akizungumza leo jijini
Dar es salaam kuhusu zoezi hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt. Mozes Kusiluka amesema kuwa Serikali imeamua kuja na
mpango huo kwa sababu ya ukubwa wa jiji hilo na wingi wa watu ulioambatana na
ujenzi wa makazi holela.
“Katika mwaka wa fedha
2016/2017 tumepanga kuwa na mpango maalum wa jiji la Dar es salaam ambapo wataalam wetu watakwenda, kuhakiki mipaka na
kupima maeneo yote ambayo hayajapimwa na kutengeneza ramani zitakazoonyesha
maeneo ya barabara na maeneo ya huduma nyingine kwa kushirikiana na wananchi
husika.
Amesema kuwa baada ya
zoezi la uhakiki Serikali itatoa hati za maeneo hayo na kusisitiza kuwa zoezi
hilo litafanyika pia katika maeneo mengine ya miji mikubwa nchini yenye watu
wengi ikiwemo jiji la Mwanza.
Dkt. Kusiluka
amesisitiza kuwa urasimishaji utakuwa shirikishi kwa kuwahusisha watu wote wa
maeneo yatakayopimwa na Serikali ambapo wananchi wenye nyumba watashirikiana na
viongozi wa Serikali katika mitaa kupanga na kuimarisha mindombinu ya maeneo
yao pamoja na kukubaliana maeneo ambayo barabara za mitaa zitapita, mitaro ya
maji machafu, magari ya kupitishia huduma za dharula kama Zimamoto nay ale ya
kubebea wagonjwa.
“Mpango wa urasimishaji
ni Shirikishi, wataalam wa ardhi watakwenda kwenye maeneo yote yatakayopimwa
hususan katika jiji la Dar es salaam na kukaa na wananchi wote,kupitia mipaka
wakishirikiana na wananchi wote kwa uwazi ili zoezi hilo liwe na manufaa na
tija kwa wananchi wote” Amesisitiza Dkt. Kusiluka.
Amesema kuwa licha ya
kuwepo kwa sheria zinazoisimamia sekta ya Ardhi
nchini Tanzania bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwemo migogoro ya Wakulima na wafugaji, migogoro ya kijinai ya mtu mm kuvunja
nyumba au kuvamia eneo la mtu bila idhini, migogoro ya mipaka kati ya majirani
na ile inayosababishwa na wananchi kutokujua sheria.
Mbali na sababu hizo
amebainisha kuwa idadi ya watu na matumizi ya ardhi kwa shughuli mbalimbali
imekuwa ikiongezeka wakati ardhi ikibakia ileile jambo linaloifanya sekta hiyo
kuja na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto hizo kupitia watalaam
waliopo.
Amesema kuwa serikali
imefanya mambo mbalimbali kuhakikisha kuwa inatatua kero za wakulima na
wafugaji katika maeneo mbalimbali kwa kuwatumia wataalam wake kupima na kupanga
maeneo ya vijiji mbalimbali, kutoa elimu pia kuajiri wataalam wa masuala ya
Ardhi katika Halmashauri zote nchini.
Aidha amesisitiza kuwa
Serikali imejipanga kupima maeneo yote ya ardhi nchini ambayo hayajapimwa
kupitia mpango wa miaka 10.
No comments:
Post a Comment