Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Enterberth Nyoni(kushoto) akisisitiza
jambo wakati wa Kikao Kazi cha Wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii
mjini Dodoma.Katikati ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bw. Erasimus Rugarabamu na
Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya
Wizara hiyo Bw.Paschal Mahinyila.
Na.Aron Msigwa - DODOMA
Wito
umetolewa kwa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo Jamii kote nchini
kushirikiana na wataalam walio katika vyuo hivyo kubuni vyanzo vipya
vya mapato kupitia uanzishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili
kuviwezesha vyuo hivyo kumudu baadhi ya gharama za uendeshaji zikiwemo
za ukarabati wa miundombinu.
Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Enterberth Nyoni ametoa wito huo
mjini Dodoma wakati aizungumza na wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii
vilivyo chini ya wizara hiyo kuhusu namna vinavyoweza kumudu baadhi ya
gharama za uendeshaji kupitia miradi mbalimbali.
"Tuna
vyuo vina maeneo makubwa ya wazi ya ardhi ambayo yangeweza kutumika
kuongeza kipato kwa shughuli za kilimo na ufugaji, maeneo haya
hayatumiki ipasavyo jambo linalosababisha wananchi wayavamie na kuanza
kulima jambo ambalo limekuwa chanzo cha migogoro baina ya vyuo husika na
wananchi" Amesisitiza Bw. Enterberth.
Amesema
kuwa licha ya vyuo hivyo kubuni miradi kujiongezea kipato, lengo la
Serikali ni kuhakikisha inaendelea kuviwezesha vyuo hivyo kwa majengo
mapya yanayoendana na hali halisi na hadhi ya vyuo husika ili kwenda na
kasi ya mabadiliko ya elimu na mahitaji ya vyuo hivyo.
Aidha,
amefafanua kuwa ipo haja ya kuangalia namna bora ya kuendelea
kuiboresha miundombinu ya vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyopo nchini
ili viendelee kuwavutia wanafunzi wanaodahiliwa kusoma katika mazingira
bora.
Amesisitiza
kuwa ni vyema vyuo hivyo kuwa na mkakati mkakati wa kujenga majengo
mapya ikiwemo madarasa ya kufundishia ili kukidhi mahitaji ya majengo,
kuhimili ushindani pia mahitaji ya makundi maalumu.
Ametoa
rai kwa wakuu hao kuangalia upya namna ya kupata fedha nje ya utaratibu
wa Bajeti ya Serikali ili kuongeza mapato yao na kuongeza kuwa Serikali
itaendelea kuvijengea uwezo vyuo hivyo kulingana na Bajeti inayopangwa
ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga shilingi
Bilioni 5.6 kwa ajili ya uendeshaji wa vyuo hivyo.
No comments:
Post a Comment