Rais Dkt. John Pombe Magufuli akimkaribisha Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Liberat Mfumukeko Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo. PICHA NA IKULU. |
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
Simu: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. John
Pombe Magufuli leo tarehe 18 Agosti, 2016 amekutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya
hiyo Balozi Liberat Mfumukeko Ikulu Jijini Dar es Salaam na kumsihi ahakikishe
Jumuiya inajielekeza kukabiliana na matatizo ya wananchi na kupunguza matumizi
ya fedha yasiyo ya lazima.
Dkt. Magufuli
amesema ni vema Jumuiya hiyo itilie mkazo katika kuziwezesha nchi wanachama
kukabiliana na matatizo muhimu ya wananchi yakiwemo upatikanaji wa maji,
uboreshaji wa miundombinu kama vile barabara na reli, kuimarisha huduma za
afya, kujenga viwanda vitakavyozalishaji ajira na kuongeza mapato, na kukuza
biashara na uwekezaji.
"Itakuwa ni
manufaa zaidi endapo nyie watendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mtafanya
juhudi kubwa kuhakikisha nchi wanachama zinajikita kukabiliana na matatizo ya
wananchi, mkifanya hivyo na mkaepuka matumizi makubwa ya fedha kwenye mambo
yasiyo ya lazima tutanufaika zaidi" Amesema
Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Dkt.
Magufuli amempongeza Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
aliyeshika wadhifa huo kuanzia Mwezi Aprili mwaka huu (2016) kwa mipango na
mikakati mizuri aliyoanza nayo katika kutekeleza malengo ya Jumuiya ikiwemo
kupunguza matumizi, kuvutia wawekezaji na kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa
miradi na programu iliyo chini ya Jumuiya hiyo.
Kwa upande wake
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Liberat Mfumukeko pamoja
kumshukuru Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwake ameahidi
kutekeleza wajibu wake vizuri na kwa manufaa ya wana Afrika Mashariki.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli ameagana na aliyekuwa Mwakilishi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya idadi ya watu
hapa nchini (UNFPA - Tanzania) Dkt. Natalia Kanen ambaye hivi karibuni
ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Msaidizi na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
UNFPA.
Dkt. Magufuli amempongeza
Dkt. Natalia Kanen kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na amesema anaamini kuwa
Dkt. Natalia Kanen atakuwa Balozi mzuri wa Tanzania hususani katika kuongeza
mkazo kwa Umoja wa Mataifa kuisadia Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo ongezeko la wakimbizi, umasikini na
huduma za mama na mtoto.
Kwa upande wake
Dkt. Natalia Kanen ambaye amekuwa hapa nchini kwa kipindi cha takribani miaka
miwili ameishukuru na kuipongeza Tanzania kwa kuwa nchi ya amani na jinsi
ilivyojitoa kuwahudumia wakimbizi kutoka mataifa mbalimbali yanayokumbwa na
matatizo ikiwemo mapigano.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es
Salaam
18 Agosti,
2016
No comments:
Post a Comment