Trending News

CCM Adverts and Promo

Saturday, August 27, 2016

Wadhibiti Ubora wa shule wanolewa kuboresha ufundishaji na ujifunzaji shule za awali, msingi na sekondari

Na: Lilian Lundo - Dar es salaam.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewajengea uwezo wadhibiti ubora wa shule 1,469 ili wapate umahiri wa kusimamia kwa ufanisi ufundishaji na ujifunzaji bora unaozingatia umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya uthibiti ubora wa shule nchini, Marystella Wasena alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mikakati ya Idara hiyo katika kukagua na kusimamia utekelezaji wa ufundishaji wa  kusoma , kuandika na kuhesabu katika shule za awali na msingi nchini.

“Kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 Idara ilifanya tathmini ya mafanikio ya utekelezaji wa mtaala ambapo shule za Msingi 6,831 zilikaguliwa na ilibainika kuwepo kwa wanafunzi 10,273 (wakiume 5,010 na wakike 5,263) wasiojua kusoma wala kuandika katika shule za Msingi 515,” alifafanua Wasena.

Marystella amesema tathmini hiyo imebainisha sababu zinazotokana na wanafunzi wenyewe kushindwa kumudu kujifunza kwa umahiri husika na sababu zinazotokana na utekelezaji wa mtaala ikiwemo ukosefu wa walimu wa kufundisha KKK.
Amesema ili kuondokana na tatizo la wanafunzi kutojua kusoma na kuandika, kila kanda na kila wilaya zimeteua shule mbili za mfano zikiwemo za Serikali na Binafsi ili kuhakikisha wathibiti ubora wa shule wanafanya ufuatiliaji wa KKK katika shule hizo kwa kutoa msaada wa kitaalamu kwa walimu kuhusiana na changamoto za ufundishaji na ujifunzaji mahiri wa KKK.

Aidha Marystella  amefafanua kuwa, Idara kupitia mpango wa LANES imeongeza idadi ya magari katika wilaya 38 yatakayotumika kwa ajili ya ukaguzi wa shule za awali, Msingi na Sekondari ambapo idara hiyo imepanga kukagua shule 8426 za awali na Msingi  na Sekondari shule 2392 ili kuona utekelezaji wa KKK pamoja na kutoa msaada kwa walimu kufundisha kwa ufasaha kulingana na malengo ya Mtaala husika.

Hata hivyo Idara hiyo ina mkakati wa kufanya tafiti mbalimbali katika shule za Awali, Msingi na Sekondari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuona utekelezaji wa Mtaala wa KKK na kutoa mapendekezo sahihi ya kuondoa changamoto na kutoa ushauri kwa Walimu, Wakuu wa Shule, Maafisa Elimu, Wamiliki wa  Shule, Kamishna wa Elimu na Wadau wa Elimu.

No comments:

Post a Comment