Cheyo ameyasema hayo leo jijini Dar es
Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu msimamo wake juu ya maandamano hayo.
“Watanzania wenzangu jambo la kuwaacha
watoto wetu kwenda kupambana na Polisi si jambo zuri, wote tupaze sauti zetu na
kusema hapana kwa maandamano ya Septemba Mosi,” alisisitiza Cheyo.
Alisema kuwa, ziko njia mbalimbali
ambazo Chadema wanaweza kuzitumia kutatua migogoro, kama vile meza ya
mazungumzo na kuachana na maandamano ambayo yanachochea vurugu na hata kutishia
amani ya nchi.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linapotoa
katazo la maandamano ni lazima utii uwepo, kwani Polisi wapo kwa mujibu wa
Sheria na Katiba. Ikiwa Chama hicho
hakikuridhika na katazo hilo basi wanatakiwa kuonana na Waziri anayehusika na
Jeshi la Polisi.
Akifafanua zaidi alisema kuwa Rais
Magufuli amekuwa akichukua hatua za makusudi za kutatua matatizo mbalimbali kama vile
kupambana na ufisadi, ambapo viongozi wengi wa Serikali wamesimamishwa kazi au
kufukuzwa kutokana na kujihusisha na
masuala ya rushwa.
Mwenyekiti huyo wa UDP amewataka
watanzania kumuunga mkono Mhe. Rais Magufuli ili aweze kutimiza ndoto zake na
yale ambayo ameyaahidi kwa ajili ya nchi ya Tanzania.
Aidha Cheyo aliwasifu viongozi wa Dini
ambao walikaa na Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kukubali kurudi bungeni bila pingamizi
lolote. Amewataka viongozi hao wa dini kuendelea kuzungumzia suala la amani kwa
Watanzania na Viongozi wa kiasa ili kudumisha amani ya nchi.
No comments:
Post a Comment