Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akizungumza na Balozi
wa Israel nchini Tanzania anayezihudumia pia nchi Afrika Mashariki za Kenya na
Uganda Mhe. Yahel Vilan (kulia) Ofisini kwake leo jijini Dar es salaam. Pamoja
na mambo mengine viongozi hao wamejadili kuhusu uanzishwaji wa ushirikiano
katika maeneo mbalimbali yatakayoinufaisha Tanzania na Israel kwenye sekta ya
Afya.
Balozi wa Israel nchini
Tanzania anayezihudumia pia nchi Afrika Mashariki za Kenya na Uganda Mhe. Yahel
Vilan (kulia)akimweleza jambo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu mara baada ya kumtembelea Ofisini kwake leo jijini
Dar es salaam.
Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu (katikati) akifurahia
jambo mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina yake na Balozi wa Israel
nchini Tanzania anayezihudumia pia nchi Afrika Mashariki za Kenya na Uganda Mhe.
Yahel Vilan (kulia) Ofisini kwake leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya Wizara hiyo, Agnes Kimemio.
Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiagana na Balozi
wa Israel nchini Tanzania anayezihudumia pia nchi Afrika Mashariki za Kenya na
Uganda Mhe. Yahel Vilan (kulia) mara baada ya mazungumzo Ofisini kwake leo
jijini Dar es salaam.Picha/Aron Msigwa -MAELEZO.
Na. Mwandishi Wetu - Dar es
Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu
amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Yahel
Vilan ambapo pamoja na mambo mengine viongozi hao wamekubaliana kuanzisha
ushirikiano katika maeneo mbalimbali ambayo yatazinufaisha Tanzania na Israel
katika sekta ya Afya.
Balozi huyo anayezihudumia
nchi za Afrika mashariki Tanzania, Kenya na Uganda katika mazungumzo na Waziri
wa Afya wa Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu ameyataja baadhi ya mambo ambayo Israel
imekua ikishirikiana na Tanzania kuwa ni pamoja na kudhamini matibabu ya moyo
kwa Watoto kupitia Taasisi ya Save Child Heart ya Israel na Mafunzo ya
madaktari bingwa na Wauguzi kutoka Hospitali mbalimbali nchini.
"Tumekuwa na
utaratibu wa kuleta madaktari ili waje watoe huduma kwa wagonjwa pamoja na
ujuzi kwa wataalam wa Tanzania" Ameeleza Balozi Vilam na kuongeza kuwa
Israel imekuwa ikitoa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalam kutoka Tanzania hususani
madaktari na Wauguzi.
Balozi huyo amesema
kuwa Israel imekua ikitoa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalam hususani madaktari
na Wauguzi kutoka Tanzania na kuongeza kuwa wanao mpango wa kusaidia
uanzishwaji wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika eneo ambalo serikali ya
Tanzania itapenda kuboresha huduma hiyo.
Kwa upande wake Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu
ameishukuru Serikali na Wananchi wa Israel kwa ushirikiano wanaouonyesha kwa Tanzania
katika eneo la tiba hususani kwenye udhamini wa matibabu ya watoto wenye
ugonjwa wa moyo katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kupitia madaktari
bingwa wanaotoka katika nchi mbali mbali ikiwemo Israel.
"Kupitia ushirikiano na Israel, Serikali tumeweza kuokoa kiasi kikubwa cha
fedha ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu, hadi sasa
kati ya wagonjwa 400 waliokuwa wanasubiri kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya
matibabu nusu yao wamepatiwa matibabu hapa nchini chini ya utaratibu huo".
Ameeleza Mhe Ummy.
Mhe. Ummy amemwomba
Balozi wa Israel kuongeza fursa zaidi za mafunzo ya fani ya Afya kwenye
kada nyingi zaidi ikiwemo kada ya wataalam wa maabara, wauguzi na madaktari.
Aidha, amemwomba Balozi wa Israel kuwezesha ujenzi wa chumba cha wagonjwa
mahututi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa - Dodoma.
Amesema hatua hiyo inatokana na uamuzi wa
serikali kuhamia Dodoma ambapo maboresho makubwa ya utoaji wa huduma za afya
yanatakiwa ili kuweza kuhudumia watu watakaohamia Dodoma.
Akikubali ombi hilo,
Balozi wa Israel Mhe. Yahel Vilan ameeleza kuwa wataalam kwa ajili ujenźi wa
chumba cha wagonjwa mahututi wanatarajia kufika nchini Tanzania mwezi Septemba
kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa ahadi ya balozi.
No comments:
Post a Comment