Trending News

CCM Adverts and Promo

Friday, September 23, 2016

NEC YAZINDUA PROGRAMU YA UTOAJI WA ELIMU YA MPIGA KURA KWA KUWAPATIA ELIMU WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA YA SONGE MUSOMA.

 Mkurugenzi Idara ya Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Emmanuel Kawishe akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe nje kidogo ya mji wa Musoma juu ya majukumu na utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa uzinduzi wa programu endelevu ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa kuyafikia makundi mbalimbali nchini.
 Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhandisi Manyiri Isaya akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe nje kidogo ya mji wa Musoma juu ya daftari la wapiga kura na namna taarifa za wapiga kura zinavyotumika kwenye chaguzi mbalimbali. Kulia ni Mkurugenzi Idara ya Huduma za Kisheria wa NEC, Bw. Emmanuel Kawishe.
 Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura wa NEC, Bi. Giveness Aswile akiwaeleza wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe  Musoma mfumo unaotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika kuwawezesha watu walio katika makundi maalum hasa watu wenye ulemavu  wenye sifa kupiga kura kupitia karatasi maalum.
 Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe iliyoko nje kidogo ya mji wa Musoma wakionesha vipeperushi na machapisho mbalimbali waliyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa lengo la kuwawezesha kuongeza uelewa juu ya majukumu ya Tume wakati wa uzinduzi wa program endelevu ya utoaji wa elimu ya mpiga kura mjini Musoma.
 Mwanafunzi wa kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe, Musoma akiwauliza swali Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (hawapo pichani) juu ya matumizi ya TEHAMA katika kuwabaini wananchi waliojiandikisha kwenye kituo cha kupigia kura zaidi ya kimoja.
 Baadhi ya wananfunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana na Songe nje kidogo ya mji wa Musoma, wakifuatilia kwa makini elimu ya Mpiga kura iliyokuwa ikitolewa na Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika shule hiyo wakati wa uzinduzi wa program ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa wananchi.
Baadhi ya wananfunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana na Songe, Musoma wakipitia machapisho mbalimbali  ya elimu ya Mpiga kura yaliyotolewa na Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika shule hiyo wakati wa uzinduzi wa program ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa wananchi. 

Na. Aron Msigwa – NEC, Musoma.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imezindua rasmi programu ya utoaji wa Elimu endelevu ya mpiga kura nchini kwa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Songe iliyoko nje kidogo ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Uzinduzi wa programu hiyo ni kuanza rasmi kwa mkakati wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata elimu ya mpiga kura ili kujenga uelewa kuhusu majukumu ya Tume , utendaji wake  na uelewa wa chaguzi mbalimbali zinazofanyika nchini.

Akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo wakati wa uzinduzi wa program hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Emmanuel Kawishe amesema kuwa NEC imeamua kuwafikia moja kwa moja wanachi ili iwapatie elimu kuhusu haki na wajibu walio nao kikatiba pia kuwajengea uelewa wa kutosha kuhusu taratibu zinazosimamia chaguzi nchini.

Amesema kuwa programu hiyo imezinduliwa kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu utendaji wa Tume na kazi za Tume ili kuongeza uelewa miongoni mwa jamii pia kuiwezesha Tume hiyo kupokea ushauri na maoni ya wananchi.

Bw. Kawishe ameeleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inalojukumu la kutoa elimu ya mpiga kura kwa mujibu wa Sheria kama ilivyoanishwa katika kifungu Na 4 (c) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 na kuongeza kuwa imeanza kuwafikishia elimu ya mpiga wananchi kura moja kwa moja katika maeneo yao.

Amesisitiza kuwa NEC imezindua programu hiyo katika shule ya Sekondari ya wasichana ya Songe ili kuwapatia fursa vijana waliotimiza umri wa kupiga kura na wale ambao bado hawajatimiza umri huo kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu chaguzi zijazo.

Aidha, amewaeleza wanafunzi hao kuwa ili mwananchi aweze kupiga kura  lazima awe amekidhi sifa na vigezo vilivyoainishwa kisheria ikiwemo kutimiza umri wa miaka 18 na kuendelea, kupiga kura katika kituo alichojiandikishia kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kifungu cha 63, kuwa na utimamu wa akili, kuwa na uraia wa Tanzania na vigezo vingine vilivyoainishwa kisheria.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhandisi Manyiri Isaya akitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya TEHAMA katika kuhifadhi na kutoa taarifa  za wapiga kura waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ameeleza kuwa matumizi ya  TEHAMA yamerahisisha utunzaji wa taarifa  za wapiga kura na kufafanua kuwa mwananchi aliyejiandikisha kwenye kituo kimoja cha kupigia kura hawezi kwenda kupiga kura katika kituo kingine.

“Napenda ifahamike kwamba kujiandikisha kwenye kituo zaidi ya kimoja kwa lengo la kupigia kura mara nyingi ni kosa kisheria na mtu huyo anashitakiwa kwa mujibu wa sheria, Tume tuna daftari la kudumu la wapiga kura tunapochakata taarifa za wapiga kura huwa tunagundua watu waliojiandikisha zaidi ya kituo kimoja, tunachofanya sisi tunachukua taarifa za kituo cha mwisho mtu alichojiandikisha” Amesisitiza.

Mhandisi Manyiri amefafanua kuwa karatasi za kupigia kura hutolewa kulingana na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha katika kituo husika hivyo hakuna namna ambayo mwananchi anaweza kupiga kura kwenye kituo zaidi ya kimoja.

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura Bi. Giveness Aswile akitoa ufafanuzi kuhusu wajibu wa Tume katika kushughulikia watu wenye mahitaji maalum hasa watu wenye ulemavu ambao wanaokidhi sifa za kupiga kura amesema kuwa Tume imekuwa ikiweka mazingira rafiki ya kuwawezesha kupiga kura.

Amesema  kuwa katika uchaguzi uliofanyika Oktoba, 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliandaa karatasi maalum za kupigia kura na maeneo wezeshi ya kupigia kura ili kuwawezesha wananchi hao kutumia haki yao ya Kikatiba kuwachagua viongozi wanaowataka.

“ Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika uchaguzi uliopita tuliweka mazingira mazuri kwa watu wenye ulemavu, na wale wasioona ambao wana uwezo wa kusoma na kuandika tukawawekea vifaa na karatasi maalum zenye nukta nundu ambazo zina majina ya wagombea wa vyama vyote ili kuwawezesha kupiga kura wao wenyewe bila msaada wa mtu yeyote” Amesisitiza Bi. Aswile.

Ameongeza kuwa NEC imekuwa ikitoa kipaumbele kwa makundi mengine hasa ya wazee, mama wajawazito kupata huduma haraka katika vituo vya kujiandikishia na kupiga kura bila kupanga mstari kama ilivyo kwa wananchi wengine.

Kwa upande wao walimu na wanafunzi wa shule hiyo wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu uzinduzi wa program hiyo katika shule yao wameishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuichagua shule hiyo kuwa ya kwanza kupata elimu ya mpiga kura.

Wamesema kuwa elimu ya mpiga kura waliyoipata kupitia kwa maofisa wa Tume na majibu ya maswali waliyouliza imewaongezea ufahamu na kuwajengea uwezo wa kuwaelimisha vijana wengine kuhusu majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wajibu wao katika kushiriki kwenye chaguzi zijazo.

Wameiomba NEC iendelea kuwapatia vijana wengi zaidi elimu ya mpiga  ili waweze kujitambua kuwa na uelewa sahihi juu ya majukumu na utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

No comments:

Post a Comment