Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inakusudia kuandaa Sera Mpya ya Sanaa kwa
lengo la kuunda sheria itakayosimamia maslahi ya wasanii nchini.
Kauli hiyo
ilitolewa jana na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nauye
alipokuwa akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara
ya Habari MAELEZO na kurushwa na Televisheni ya Taifa (TBC 1).
“Sera ya Utamaduni iliyopo sasa ina mapungufu
kwani haijaeleza vizuri namna inavyowanufaisha wasanii na kusimamia kazi zao '’ Alisema Mhe. Nape.
Alisema wizara inaendelea na
mchakato wa kuandaa Sera ya Sanaa ambayo itakuwa suluhisho katika uundaji wa
sheria nzuri itakayosimamia kazi za wasanii na kubainisha kuwa mchakato huo utawashirikisha wadau mbalmbali.
Mhe. Nape
alieleza kuwa serikali inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali zinazowakabili
wasanii katika uendeshaji wa biashara zao, hasa kipato kidogo kisichoendana na
kazi zao, kazi zao kuingiliwa na watu wasiohusika ambao wamekuwa wakijinufaisha wenyewe na uuzwaji
holela wa kazi za wasanii kutoka nje nchini.
Aliongeza
kuwa ili kudhibiti vitendo hivyo wizara kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na
usalama imekuwa ikiendesha msako katika maeneo mbalimbali ili kuwabaini na
kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria wale wote wanaohujumu kazi za wasanii hapa nchini.
Kuhusu Sekta
ya Utamaduni alisema kuwa watanzania wanapaswa kujenga utamaduni wa kujituma na
kuacha tamaduni ambazo ni kinyume na maadili ya mtanzania hasa vitendo
vya ukeketaji kwa watoto wa kike, ndoa za utotoni na baadhi ya wazazi kutosomesha
watoto wa kike.
Aidha,alisema
kuwa lugha ya Kiswahili inaendelea kukua kwa kasi kwa kuwa ni lugha ya kumi
duniani na kuongeza kuwa bunge la Afrika Mashariki limepitisha azimio la kuitambua na kutumia
lugha hiyo katika mikutano yake.
Alitoa wito kwa wataalam wa lugha ya Kiswahili
kuandika vitabu vingi zaidi vitakavyosaidia kuikuza lugha hiyo pia wasanii
kwenda katika vyuo vya sanaa kupata utaalam utakaowawezesha kufanya kazi zao katika
ubora na mvuto zaidi.
No comments:
Post a Comment