Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
Na Ismail Ngayonga - Dar es Salaam.
SERIKALI inakusudia
kuwapeleka katika kambi za mafunzo ya Jeshi la Kuujenga Taifa (JKT) watoto wa mitaani wenye
umri wa zaidi ya miaka 18 ili wajifunze stadi za kazi na shughuli za uzalishaji mali.
Hayo
yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy
Mwalimu wakati wa mahojiano maalum
katika kipindi cha Tunatekeleza kinachoandaliwa na Idara ya Habari (MAELEZO) na
Televisheni ya Taifa (TBC1).
Waziri
Ummy amesema hatua hiyo inalenga kuliwezesha kundi hilo la vijana kujihusisha na
shughuli za uzalishaji mali badala ya kuzurura hovyo mitaani sambamba na
kujihusisha na tabia na vitendo vinavyokiuka maadili katika jamii.
Amesema tayari watendaji wa Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Waziri Mkuu tayari
wamekutana kujadiliana kuhusu suala hilo ili kuangalia namna bora zaidi ya kusadia
kundi hilo.
Amefafanua kuwa
vituo vingi vya kulelea watoto hao vimekuwa na watoto waliozidi umri wa miaka
18, ambapo kwa mujibu wa sheria hawatakiwi kuwa katika vituo hivyo na kuongeza kuwa
ofisi yake itahakikisha zoezi la kuwapeleka katika mafunzo hayo
linatekelezeka.
Katika
hatua nyingine Waziri Ummy amepiga marufuku tabia za baadhi ya watu, asasi na
vikundi kuanzisha vituo vya kulea watoto yatima pasipo kuwa na usajili kwani
kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kwa
mujibu wa Waziri Ummy amesema tayari ofisi yake imetoa maelekezo kwa Kamishina
wa Ustawi wa jamii kufanya tathimini na utafiti wa kina kuhusu vituo vya kulea
watoto yatima, ambapo iwapo kutabainika vituo vitakavyokosa sifa hatua za
kisheria zitachuliwa kwa wahusika.
Kuhusu
chanjo, Waziri Ummy amesema Serikali itaanza kutoa chanjo ya saratani ya shingo
ya kizazi kwa watoto wenye umri wa miaka 9-13 ili kukabiliana na changamoto ya
maradhi hayo nchini.
Waziri
Ummy amewataka wazazi kutoa ushirikiano pindi zoezi hilo litakapoanza kwa
kuwa halitakuwa na madhara ya kiafya kwa watoto wao.
Aidha, amesema Serikali imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha fedha kila mwaka kwa ajili
ya matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi kwa
akina mama ambayo inaambukizwa na virusi vinavyojulikana kwa jina la Human Papiloma Virus (HPV).
“Tumeamua
kuteua kundi la watoto wa lika huo kwani wengi wao katika umri huo wanakuwa
bado hawajaanza kujihusisha na vitendo vya mapenzi” amesema Waziri Ummy.
Amesema
katika bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali imepanga kuipatia taasisi ya saratani
ya ocean road kiasi cha Tsh. Bilioni 3
kwa ajili ya ununuzi wa madawa, ikilinganishwa na kiasi cha Tsh. Milioni 600
zilizokuwa zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2015/16.
Akizungumzia
changamoto iliyojitokeza hivi karibuni ya ukosefu wa chanjo katika vituo vya
huduma ya hivi nchini, Waziri Ummy amesema suala hilo litakuwa historia hivi
karibuni kwani tayari Serikali imeagiza kutoka nje ya nchi baadhi ya chanjo
hizo.
No comments:
Post a Comment