Trending News

CCM Adverts and Promo

Friday, March 18, 2016

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAIPONGEZA TPA NA KUITAKA BANDARI IJIENDESHE KISASA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kufunga mitambo ya kisasa ya kiulinzi bandarini. 

Aidha imetoa wito kwa Serikali kuendelea kuijengea uwezo Bandari ili iendelee kujenga uwezo miundombinu ya kisasa ili kuiwezesha Bandari kukabiliana na ushindani wa bandari zilizo nchi za jirani.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo mara baada ya Kamati hiyo kutembelea eneo la TPA na kukutana na viongozi na watendaji wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Dkt. Norman Adamson Sigalla amesema kuwa  ufungaji wa mitambo ya kisasa ya kiulinzi  (Integrated Security System - ISS)  utaongeza ufanisi bandarini.

Kwa upande  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Alois Matei akiuelezea mfumo huo wa ulinzi amesema ni moja ya juhudi zilizofanywa na mamlaka hiyo kulihakikishia ulinzi  eneo lote la TPA.

Amesema ISS ni mfumo wa kisasa wa kiulinzi unaohusisha uwekaji wa nyaya maalum katika uzio wa bandari, kutengeneza mageti ya kisasa ambapo katika sehemu hiyo mitambo itakuwa na uwezo wa kuchukua kumbukumbu za wale wote wanaoingia na kutoka katika maeneo ya TPA ikiwa ni pamoja na magari.

Mfumo huo mpya wa kiulinzi pia unahusisha ufungwaji wa kamera 486 katika maeneo yote ya bandari, ukiwa ni mkakati wa Mamlaka kutengeneza jicho la tatu katika mpango wake wa kudhibiti wizi bandarini.
Pamoja na mradi huo wa ISS, Mamlaka imekuwa na mikakati mbalimbali ya kudhibiti wizi  ndani ya eneo la bandari.

Akielezea hali ya utendaji kazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania  kwa Wajumbe wa Kamati hiyo, amesema kuwa hali ya utendaji kazi katika kipindi cha miaka mitano ilikuwa ya mafanikio.

Mhandisi Matei alifafanua kwamba mafanikio yaliyopatikana katika kipindi husika ni pamoja na kuongezeka kwa shehena ya mizigo na mapato.

Katika kipindi cha 2014/2015 shehena iliyohudumiwa na bandari za Mamlaka ilikuwa tani 15,979, 693 ambazo ni ongezeko la tani 551,863, sawa na asilimia 3.6 ikilinganishwa na tani 15,427, 830 zilizohudumiwa mwaka 2013/2014.

Kwa upande wa mapato, ziada imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 21.8 kwa mwaka ambapo mwaka 2014/2015, Mamlaka ilipata ziada ya shilingi za kitanzania 214,663.62 milioni kutokana na mapato ya shilingi za kitanzania 679,316.95 milioni na matumizi ya kawaida ya shilingi za kitanzania 464,653.32 milioni.




No comments:

Post a Comment