Trending News

CCM Adverts and Promo

Thursday, August 4, 2016

SERIKALI YATANGAZA KIAMA KWA MADEREVA WALEVI NA WAZEMBE


Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Mhe. Injinia Yusuf Hamad Masauni akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mkakati wa miezi sita wa baraza hilo wa kukabiliana na ajali za barabarani mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Naibu Kamishna Mohamed Mpinga.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Naibu Kamishina Mohamed Mpinga akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mkakati wa miezi sita wa baraza hilo wa kukabiliana na ajali za barabarani mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Mhe. Injinia Yusuf Hamad Masauni.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Mhe. Injinia Yusuf Hamad Masauni (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa mkakati wa miezi sita wa baraza hilo wa kukabiliana na ajali za barabarani mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Usalama Barabarani na Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra), Geofrey Silanda akijibu swali kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mkakati wa miezi sita wa baraza hilo wa kukabiliana na ajali za barabarani mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Eliphace Marwa 
Na Jonas Kamaleki
Serikali yajipanga kupunguza ajali za barabarani kwa kiwango cha takribani asilimia 10 hapa nchini ili kupunguza vifo na majeruhi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Yusuf Hamad Masauni  kuwa baraza la Usalama Barbarani linakerwa sana na kadhia ya ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.

“Kukithiri kwa ajali za barabarani kwa siku za hivi karibuni, umewezesha Baraza kuibuka na Mkakati wa Miezi Sita (6) unaolenga katika kukabiliana na ajali za barabarani nchini, mkakati huu ni wa muda mfupi kuanzia mwezi Agosti, 2016  hadi Februari 2017 tutakapokaa na kutathmini matokeo yake”, alisema Masauni.

Masauni amesema ajali za barabarani zimewaacha watoto wakiwa yatima  na kuwafanya akina mama kuwa wajane, hivyo  juhudi za makusudi inabidi zifanywe ili kupunguza kama sio kuondoa kabisa ajali hizo.

Ametaja vyanzo vikuu vya ajali za barabarani nchini kuwa ni pamoja na Makosa ya Kibinadamu, mazingira ya barabara na ubovu wa vyombo vya moto.

Naibu waziri huyo amesema takwimu za ajali barabarani katika miaka mitatu tangu 2012 ajali ziliongezeka toka 23,578 hadi 23, 842 kwa mwaka 2013, vifo vilikuwa 3,969 kwa mwaka huo hadi kufikia 1,043 mwaka 2013. 

Vifo hivyo vilipungua hadi kufikia 3,760 mwaka 2014, upungufu huo ulitokana na usimamiaji madhubuti wa Sheria na kanuni za Usalama barabarani pamoja na juhudi zilizofanya na Baraza kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Kwa mujibu wa Masauni, Mkakati uliozinduliwa unalenga kudhibiti makosa yanayosababisha madhara makubwa na ambayo husababisha kuongezeka kwa ajali za barabarani.

Ameyataja mambo hayo kuwa udhibiti wa madereva walevi na kuendesha kwa uzembe, mwendokasi kwa madereva na wamiliki wa magari, uendeshaji magari bila sifa au leseni za udereva na Bima.
Masauni  ametaja mambo mengine katika Mkakati huu kuwa ni kudhibiti usafirisha wa abiria kwa kutumia magari yasiyo na sifa kama vile Noaha na Probox, ajali za pikipiki za magurudumu mawili (bodabaoda) na matatu (bajaj) na kuhakikisha abiria wanafunga mikanda ya usalama wanapotumia vyombo vya moto kwa ajili ya usafiri.

Maeneo mengine yatakayoangaliwa kwa mujibu wa Masauni ni kuyabaini na kuyadhibiti maeneo tete na hatarishi ya ajali za barabarani (Black spots/kilometres), kuangalia uwezekano wa kufanya marekebisho ya Sheria za Usalama barabarani, kuanza utaratibu wa Mfumo wa Nukta (point system) kwenye leseni za udereva, kutoa mafunzo msasa kwa askari wa usalama barabarani na kutoa elimu na mafunzo kwa bodaboda.


Ili kupunguza ajali za barabarani, Masauni amasema Mkakati utadhibiti vitendo vya rushwa ambapo watoaji na wapokea rushwa wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria, kuwapa tuzo askari wanaofanya vizuri kuzuia ajali na kuwahusisha wamiliki wa magari ya abiria nay a mizigo, katika kuutekeleza mkakati.

No comments:

Post a Comment